Rais Kenyatta kuongoza hafla ya kutoa rasmi ripoti ya BBI kwa umma

Rais Uhuru Kenyatta leo ataongoza hafla ya kutoa rasmi ripoti ya Mpango wa Kuwaunganisha Wakenya BBI kwa umma katika uwanja wa Bomas jijini Nairobi.

Ripoti hiyo iliwasilishwa kwa Rais na jopo lililoitayarisha likiongozwa na mwenyekiti wake aliye pia Seneta wa Garissa Yusuf Haji katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Nairobi hapo jana.

Kupitia ripoti hiyo Wakenya watapata fursa ya kuboresha nchi kwa kuimarisha mfumo wa utawala na pia kuwaunganisha Wakenya kwa kuimarisha utangamano kati ya jamii zote nchini.

Wakenya wanatarajiwa kuisoma ripoti hiyo na kuijadili kwa makini na busara kabla ya kuamua kuiunga mkono au kuipinga.

Viongozi mbalimbali wa kisiasa, kidini na kijamii, mashirika mbali mbali na maafisa wakuu serikalini wanaendelea kuwasili Bomas kuhudhuria hafla hiyo.

 -PSCU