Katibu mkuu wa Jubilee Raphael Tuju bado yuko ICU

Madaktari wanaendelea kuifuatilia hali ya katibu mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju, ambaye amelazwa katika hospitali ya Karen. Tuju yuko katika chumba cha wagonjwa mahututi, baada ya kuhusika katika ajali iliyotokea jumatano asubuhi kwenye barabara kuu ya Nairobi-Nakuru.

Hayo yakijiri, mahakama hii leo itaskiza kesi ambapo aliyekua waziri wa michezo Rashid Echesa anashtakiwa kwa makosa ya ulaghai. Echesa alikamatwa jana na magari yake kunaswa kabla ya kuwasilishwa kwa makao makuu ya DCI na kuhojiwa kwa masaa kadha.

Kwingineko, ripoti kuhusu mauaji ya kiholela yanayotekelezwa na polisi, yaliyoripotiwa mwaka 2019, itatolewa hii leo na mashirika ya kutetea haki za binadamu IMLU, Amnesty International na Justice Mission.

Ramadhan Rajab kutoka Amnesty International anasema ripoti hio itaambatana na zoezi la kuwapa maua ya siku ya wapendanao jamii za waathiriwa wa ukatili wa polisi na kusambaza ujumbe #SpreadRosesNotBullets.

Masuala ya afya ya akili yanapaswa kushughulikiwa mapema, ili kuhakikisha kuwa hayazidi kudorora na kufikia hali mbaya.

Seneta Sylvia Kasanga anasema ni muhimu kutafuta usaidizi iwapo hujihisi vizuri huku akiongeza kwamba serikali inafaa kukabiliana na unyanyapaa unaohusishwa na maradhi ya akili, kama vile tu ilivyokabiliana na unyanyapaa dhidi ya HIV katika miaka ya tisini.