Nafasi ya Kiswahili katika jamii, Kongole Radio Jambo - Sairin Lupia

Na Sairin Lupia

Profesa Majisifu, stashahada ya Kiswahili, Chuo kikuu cha London. Sadfa iliyoje? Hii ndio hali katika Afrika huru. Kiswahili ambayo ndio lugha yetu waafrika, sasa sisi twaenda kwa mzungu kutufundisha lugha yetu ya mama.Tumelaliwa kimawazo na hata masomo ya vitu ambavyo tunavifahamu tumewaachia wengine kutufunza.

Nafasi ya Kiswahili katika bara la Afrika na hata humu nchini ni nafasi kubwa sana. Kiswahli ndio lugha ambayo inazungumzwa na waafrika wengi sana nyuma ya kiarabu katika bara letu. Lakini sisi kama waafrika tumezipa kipaumbele lugha zingine tulizoachiwa na wakoloni. Katika Afrika huru, kuzungumza kiingereza, kifaransa au kijerumani ni jambo la kujivunia sana kuliko mtu anayezungumza lugha asili au Kiswahili, Kiswahili kimedunishwa. Wasomi wetu waenda ng’ambo kufunzwa lugha hii yetu ya Kiswahili. Sisi wenyewe tumefanya Kiswahili kushushwa hadhi hata kwa jumuiya ya mataifa, tukisahau hii ndio lugha ya kutuunganisha sisi. Taifa la Rwanda limepiga hatua muhimu kwa kuidhinisha Kiswahili kuwa lugha ya taifa.

Ulikuwa mwaka wa 1974, ambapo Kiswahili kilifanywa lugha ya taifa humu nchini. Hii ilikiwa miaka kumi baada ya kupata uhuru. Iliwachukua viongozi wetu miaka kumi kuona kwamba Kiswahili kinafaa kuwa lugha ya taifa. Siku hiyo tulijionea maajabu ya Musa katika bunge huku wabunge wakijaribu kukiongea Kiswahili. Ni jambo la kusikitisha ya kwamba viongozi waliona vizuri kujifunza lugha ya mkoloni bali sio lugha ya mwananchi, kwa kweli tulitawaliwa kiakili. Katika nchi mbalimbali kama Tanzania, walichagua kukiendeleza Kiswahili na shida za ukabila ni nadra sana ikilinganishwa na nchi zingine katika bara la Afrika. Tanzania ina lugha asili karibu mia, lakini wote wanaunganishwa na Kiswahili. Basi hata ukitoka Dodoma hadi Arusha lugha ni Kiswahili.

Kama nchi ninaamini tunafaa kukiendeleza Kiswahili na kukisaidia kuchukua nafasi yake inayofaa katika jamii. Nikiwa shuleni nakumbuka vizuri katika fasihi andishi tulifunzwa kuhusu mbinu za kuendeleza Kiswahili. Jukumu la bodi ya Kiswahili nchini, lakini kazi ya bodi hii haionekani. Kutoka kwa uongozi duni hadi kwa ukosefu wa fedha za kufanikisha mipango yake. Ni mambo kama haya ambayo yanaonyesha jinsi serikali imetelekeza Kiswahili. Katika katiba ya Kenya, Kiswahili ni lugha ya taifa lakini ni nadra sana lugha hii itumiwe na wabunge wetu wakitoa hoja zao bungeni.

Sio tu katika uzungumzaji wa Kiswahili , hata kwa uandishi na uanahabari Kiswahili bado hakithaminiwi. Bado tuna magazeti machache mno nchini yanayochapishwa katika lugha ya Kiswahili. Katika taarifa za mitandaoni ni tuvuti ya Radio Jambo pekee inayopiga hatua katika uchapishaji wa taarifa na matukio katika lugha ya Kiswahili. Hali hii imechangiwa pakubwa na wakenya kutokifahamu Kiswahili vyema , wengi huiona kama lugha ngumu.

Kusoma maandishi kama haya ya Kiswahili kwa wakenya wengi ni kibarua cha ziada kuliko kimombo. Hii ni licha ya wakenya wote kukisoma Kiswahili katika shule za msingi na upili. Ni jukumu la serikali kukifanya Kiswahili kuwa lugha itakayopendwa na kuenziwa na wakenya. Katika uanahabari na uandishi itakuwa vyema kwa washikadau kukuza na kuendeleza matumizi ya Kiswahili. Kuwekeza katika majarida na mitandao ya kukuza Kiswahili kutasaidia sana kupiga jeki lugha hii.

Ningependa kuwapa kongole Radio Jambo kwa harakati zao za kuendeleza lugha hii hasa miongoni mwa waandishi na wanahabari wanaochipuka. Kwa kuendeleza na kukuza vipaji miongoni mwa vijana wetu kwa kuwapa nafasi ya kuandika katika lugha hii, Radio Jambo inakuza lugha hii ya taifa. Mimi mwenyewe kama mwandishi ibuka ninazo shukran kemkem kwao kwa nafasi hii. Ni katika harakati kama hizi na mashirika kama haya ndiposa Kiswahili kitarejesha hadhi yake katika ulingo wa kimataifa. Serikali na taasisi za elimu zinafaa kushirikiana na wadau kama Radio Jambo ili kuona vile Kiswahili kitakuzwa.