Mcheshi wa Churchill Show, Othuol Othuol alazwa KNH baada ya kuzirai

Mcheshi wa Churchill Show, Othuol Othuol amelazwa katika hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta. Msanii huyo wa ucheshi ambaye hii maajuzi alikuwa akiugua Kifua Kikuu(TB), alilazwa katika hospitali hiyo Jumatano, Juni 24 asubuhi, ambapo alihamishwa kutoka kwa hospitali moja ya Kitengela.

Duru za habari  zinaarifu kuwa mcheshi huyo alizirai Jumanne Juni 23, akiwa nyumbani kwake na alikimbizwa katika hospitali iliyokuwa karibu kabla ya kutumwa KNH.

Baadhi ya marafiki zake walisema kuwa  Othuol alitengwa kwa zaidi ya saa 24 akisubiri kushughulikiwa KNH kwa sababu ya foleni ndefu.

Mmoja wa maswaiba wake aliyetambuliwa kama Ken Waudo(Meneja wa Churchill Show ), Katika ujumbe mrefu kwenye Facebook alikashifu hospitali hiyo kwa kushindwa kumlaza Othuol kwa mintarafu ya foleni ndefu. Aliomba umma kuchangisha msaada kupitia mitandao ya kijamii ili kumsaidia Othuol alazwe.

Hata hivyo, Othuol alilazwa dakika chache baadaye kufuatia kampeni iliyoendeshwa mtandaoni na baadhi ya marafiki zake.

Hali yake ya sasa ya afya inakujia yapata miezi saba baada ya kuugua kifua kikuu. Othuol alikuwa amegura uwanja wa ucheshi ili aweze kupata nafuu lakini alirejea mara tu alipopona.

Mchekeshaji huyo ni miongoni mwa maelfu ya wacheshi na waigizaji ambao walipokea KSh 10,000 hii maajuzi kutoka kwa serikali ili kuwalinda wakati huu wa janga la virusi vya corona.