Madereva 15 wa trela kutoka Kenya walio na Covid 19 wazuiwa kuingia Uganda

Truckers
Truckers
Madereva 15 wa Kenya  wamezuiwa kuingia nchini Uganda kwa sababu ya COVID 19.  15 hao walipatikana na virusi hivyo baada ya kupimwa  katika eneo la Malaba, Busia  na hawakuruhusiwa kuingia Uganda.

Ni miongoni mwa  raia 19 wa kigeni wakiwemo watanzania wawili  na raia wawili wa DRC waliopatikana na ugonjwa huo katika kituo hicho cha mpakani.

" Kuingia kwao nchini Uganda hakujaruhusiwa"  taarifa kutoka mamlaka za Uganda imesema.

Uganda imesema matokeo ya vipimo  vyao vilivyofanywa Julai tarehe 14  vimethibitisha visa vitatu zaidi vya ugonjwa huo.

Kati ya visa hivyo vitatu, viwili ni vya raia wa Uganda  waliowasili kutoka Kenya katika mpaka wa Busia ilhali  kisa kingine ni kutokea Kampala. Uganda hadi kufikia sasa ina visa 1,043.

Mwezi  Mei  waziri wa  afya Uganda alipunguza idadi ya walio na virusi hivyo baada ya rais Yoweri Museveni kuagiza kuondolewa kutoka orodha hiyo kwa madereva wote wa kigeni waliopatikana na ugonjwa huo .