Uhuru azindua mradi wa shilingi bilioni 1.9 wa madawati ya shule yanayoundwa nchini

Rais Uhuru Kenyatta siku ya Alhamisi alizindua mradi wa shilingi bilioni 1.9 wa madawati ya shule ambapo maseremala watauza madawati 650,000 yanayoundwa humu nchini.

Mbali na kutoa vifaa kwa shule za sekondari na zile za msingi, mradi huo ambao ni sehemu ya mpango wa serikali wa kufufua uchumi baada ya janga la Covid-19 unalenga kuimarisha sekta ya jua kali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo katika karakana ya useremala mtaani Umoja, Kaunti ya Nairobi, Rais Kenyatta alisema mradi huo umeandaliwa kwa msingi wa mpango wa ajira wa Kazi Mtaani unaoendelea.

“Baada ya mpango wa Kazi Mtaani, tumesema badala ya madawati ya shule yanayoundwa na makampuni makubwa, tutawapa vijana wetu nafasi ya kutumia maarifa yao," rais alisema.

“Tuna imani kwa watu kujipatia riziki kutokana na jasho lao na hivyo tuliamua kuwapa nafasi vijana wetu wenye maarifa kupata riziki ya hadhi maishani,” kasema Rais.

Kiongozi wa Taifa alisisitiza kujitolea kwake kuendelea kuimarisha maisha ya Wakenya wote kwa kuweka mazingira yanayofaa kwa raia wenye bidii kujiimarisha.

“Sitaki kujihusisha na siasa duni za kuitana majina. Badala yake, nafanya bidii kuhakikisha Wakenya wote wanafanya kazi na kufurahia matunda ya kazi zao,” kasema Rais.

Rais aliamrisha Wizara ya Elimu na ile ya Usalama wa Ndani kuhakikisha kwamba miradi hiyo inawanufaisha maseremala kote nchini.

“Tunataka kuhakikisha vijana wetu wote wenye maarifa wanahusishwa ili kunufaika kutokana na jasho lao. Mradi huu sio wa Nairobi pekee bali wa Wakenya wote wenye maarifa na wanahudumu katika sekta ya jua kali,” kasema Rais.

Alitoa changamoto kwa maseremala wa humu nchini kuhakikisha wanaunda na kuuza madawati yanayotimiza viwango vya ubora wa juu na akashauri watakaonufaika na mradi huo kubuni vyama vya ushirika vya akiba na mikopo ili kuongeza mapato yao kutokana na mradi huo.

“Mara tu mtakapoanza hii kazi, himizeni vijana wote kubuni vyama vya ushirika ambapo wataweza kuweka akiba yao. Msitumie kila shilingi, ni jambo la busara nyinyi kujiwekea akiba kwa manufaa ya siku za baadaye,” kasema Rais.