Mbunge Oscar Sudi ashtakiwa huku akiondolewa mashtaka matatu

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi alishtakiwa rasmi siku ya Jumatano na kufunguliwa mashtaka matatu huku mashtaka mengine yaliyokuwa yamependekezwa dhidi yake yakiondolewa.

Upande wa mashtaka uliondoa mashtaka ya kukataa kutiwa mbaroni, kumiliki mbunduki kinyume cha sheria na kumshambulia afisa wa polisi.

Sudi sasa atajibu mashtaka mawili ya kutoa matamshi ya uchochezi na uchokozi.

Hakimu mkuu wa Nakuru Lilian Arika hata hivyo alikataa ombi la Sudi kupitia wakili wake akitaka kuruhusiwa kuhutubia mikutano ya kisiasa.

Mahakama iliyongeza muda wa marufuku ya mbunge huyo kuhutubia mikutano ya kisiasa akisubiri kusikizwa kwa kesi yake Oktoba 6.

Sudi alijisalimisha kwa polisi wiki mbili zilizopita baada ya kudaiwa kwenda mafichoni alipokuwa akisakwa na polisi. Kwa wakati mmoja kulikuwa na patashika nyumbani kwake wakati maafisa wa polisi walipokwenda nyumbani kwake usiku wakitaka kumkamata. Katika patashika hilo afisa wa polisi anasemekana kujeruhiwa.

Mbunge huyo aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi nusu milioni baada ya mahakama kuu kubatilisha uamuzi wa mahakama ya chini iliyokuwa imemnyima mbunge huyo dhamana kwa misingi kwamba kuachiliwa kwake kungevuruga amani.