Unaweza kuwa wa kwanza kutupa mistari,wanadada mwongozo ndio huu

Kunao msemo kwamba  anayeuliza ni mjinga wa dakika tano lakini anayekosa kuuliza atasalia mjinga   maisha yake yote .Ndio  usemi ambao unafaa kukupa taswira ya jinsi mambo yatakavyokuwa endapo kama mwanadada utapatwa na woga wa kuwa wa kwanza kuzungumza na  mwanamme ambaye umevutiwa naye .

 Katika  hali ya kawaida na kutokana na  mazoaea au mila na desturi , inafahamika kwamba mwanamme ndiye humtongoza mwanammke ,lakini usasa na kubadilika kwa mambo pamoja na teknolojia  ni mambo ambayo yamesAwazisha  uwanja  na wanawake sasa wanapata ujasiri wa kuwakaribia wanaume na hata kuanza mchakato wa kuwajua  na hata kuwatongoza .

Je ,ni vipi  unavyoweza kuwa wa kwanza ‘kutupa mistari’ na kufaulu ?

Hatua kwa hatua

Siri  unayofaa kufahamu kama mwanamke ni kwamba iwapo wewe utatangulia kuzungumza na mwanamme ambaye amekuvutia fahamu kwamba ni bora upige  hatua moja hadi nyingine .Usije ukamshtukiza kwa kumwagia  moyo wote wakati mmoja kwani hilo litampa mshtuko na atarudi nyuma .Mwanzo hakikisha kwamba mnafahamiana kama marafiki lakini unapozungumza naye hakikisha anafahamu kwamba kwa kweli unampa muda wako .Hilo litamuacha na fikra za picha na sura yako akilini na hata huenda akachukua mwongozo kutoka hapo na akumalizie kazi . ni heri kuanza kama rafiki yake na umkaribie hadi upate wepesi wa kumweleza kwamba anakuvutia  ama unampenda kwa njia Zaidi ya urafiki

Ucheshi na kujiamini

Ingawaje  kuna dhana kwamba wanaume hupenda kuwinda na hivyo basi wao ndio hupendelea kutongoza kwanza ,iwapo kama mwanamke unafahamu jinsi ya kumfanya apasue kicheko na ujiamini hata katika mazungumzo yako ,basi safari yako kuuteka moyo wake itakuwa  rahisi sana .Kuna wanawake wenye uwezo wa kuzua bashaha katika nyuso za wanaume na wao hupata urahisi sana wa kuanza mchakato mzima wa kujinyakulia mwanamme .

Muulize maswali

Unapotaka kujua mengi kuhusu mwanamme ,yeye hupatwa na mwamko wa kutaka kujua mbona una hamu sana ya kumjua na hiyo ni njia tosha ya kumfahamiha kwamba upo  na una nia Zaidi ya moja . Wanaume hupenda sana wakati mwanamke ana uchu wa kutaka kuwajua kwa undani na  akiipokea vyema ishara hiyo ya maswali basi atafunguka na itakuwa rahisi wewe kuwasiliana naye .

Usijitupe

Wakati mwingine wanawake wanaovutiwa na wanaume huanza kupoteza utaratibu kwa sababu ya haya au kutojiamini na kujipata wakijitupa kwa mwanamme .Hilo bila shaka litampa  hofu kwa sababu ataanza kushangaa umejitupa hivyo kwa wanaume wangapi hata kama sio kawaida yako kujipata  katika hali kama hizo

 Tabasamu

Tabasamu ni kitu kinachozungumza mengi na  inafahamika kwamba tabasamu nzuri ya mwanamke hufungua roho hata ya mwaname ambaye kwa mbali anaweza kuonekana mkali au mgumu wa kuzungumza naye .Kama mwanamke jifunze ustadi wa kupiga tabasamu nadhifu sana ambayo inamuacha mwanamme hoi .Kuna wanawake waliopendwa kwa kutabasamu tu hata bila kutamka neno !