Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amewasuta baadhi ya wanasiasa wanaomshinikiza kutangaza mipango yake ya 2022 kabla ya kura ya maoni kufanyika.
Raila anasema atatangaza nia yake wakati unaofaa.
Hayo yakijiri, mbunge wa Dagoretti Kaskazini Simba Arati na mwenzake wa Mugirango Kusini Sylvanus Osorowa mesameheana kufuatia tukio la Februari Mosi walipopigana mangumi katika mazishi waliyokuwa wamehudhuria katika kaunti ya Kisii.
Wawili hao waliweka tofauti zao kando kwa kusalimiana jana wakati wa mazishi ya mbunge wa Bonchari Oroo Oyioka huko Kisii.
Tukielekea mahakamani, mwanaume aliyemnyonga hadi kufa msichana wa miaka mitatu baada ya kumnajisi miaka mitatu iliyopita katika kijiji cha Chemorut huko Bomet amehukumiwa kifo na mahakama moja ya Bomet.
Mahakama ilisema kuwa ilitambua kuwa hukumu ya kifo ilifutiliwa mbali ila kumpa adhabu nyingine kungekiuka kile jamii inayoamini kuwa haki.