Chama cha Jubilee kuwaadhibu wawakilishi wadi waliopiga teke BBI-Kuttuny asema

Muhtasari
  • Naibu katibu mkuu wa Jubilee Joshua Kuttuny anasema chama hicho kitawaadhibu zaidi ya wawakilishi wadi  20 ambao walitenda kinyume na katiba ya chama 
  • Alikuwa akizungumza huko Eldoret baada ya kumpokea mgombea wa chama hicho Lucy Chomba ambaye alishinda katika uchaguzi mdogo wa wadi ya Huruma
Image: Mathews Ndanyi

Naibu katibu mkuu wa Jubilee Joshua Kuttuny anasema chama hicho kitawaadhibu zaidi ya wawakilishi wadi  20 ambao walitenda kinyume na katiba ya chama kwa kupiga kura dhidi ya BBI katika mabunge ya kaunti.

Kuttuny anasema tayari walikuwa wamepokea malalamiko juu ya wawakilishi wadi katika maeneo mengine ikiwa ni pamoja na kaunti ya Elgeyo Marakwet ambapo Gavana Alex Tolgos alikiandikia chama hicho juu ya utovu wa nidhamu na baadhi ya wawakilishi wadi wa kaunti hiyo.

"Tumepokea malalamiko juu ya mwenendo wa wawakilishi wadi na tuko katika mchakato wa kuwahudumia ili waeleze ni kwanini walienda kinyume na chama ambacho kimewafanya wafike mahali walipo," Kuttuny alizungumza.

Alikuwa akizungumza huko Eldoret baada ya kumpokea mgombea wa chama hicho Lucy Chomba ambaye alishinda katika uchaguzi mdogo wa wadi ya Huruma.

"Chama kina katiba yake na tuna kamati ya nidhamu ambayo itashughulikia suala hilo hivi karibuni," alisema Kuttuny.