Spika wa zamani wa bunge la kaunti ya Nairobi Alex Ole Magelo aaga dunia

Spika wa zamani wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Alex Ole Magelo ameaga dunia.

Magelo alifariki kufuatia kuugua kwa muda mfupi katika Hospitali ya Nairobi, gavana wa Kajiado Joseph Ole Lenku amethibitisha.

"Ni kwa moyo mzito kwamba ninatangaza kifo cha mmoja wa wana wetu shujaa wa jamii yetu. Marehemu Magelo alifariki katika Hospitali ya Nairobi ambapo amelazwa kwa wiki kadhaa sasa," Lenku alisema.

"Kifo kimetunyang'anya mtu shujaa na wa kutegemewa, fadhili, msimamizi wa mpira, mwanasiasa, na mtumishi wa umma aliyejitolea ambaye umaahiri wake katika maswala ya jamii ulimwezesha kusugua mabega na watu wa hali ya juu na hodari katika nchi hii katika hatua tofauti za maisha yake."

Magelo ambaye alikuwa msimamizi wa zamani wa AFC Leopards alikuwa akisimamia Leopards wakati kilabu ilifuzu kupandishwa ngazi ya ligi kuu mnamo 2009.

Baada ya kuondoka kwa Leopards, Magelo alijiingiza katika siasa, akihudumu kama Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi, kutoka 2013 hadi 2017.

Mwaka jana, Magelo alijiondoa kwenye kinyang'anyiro cha spika wa bunge la kaunti ya Nairobi  na kumuunga mkono spika wa sasa Benson Mutura.