Mke na watoto wa Gavana Mohammed Abdi hawatatoa ushahidi katika kesi ya mashtaka dhidi yake-Kamati

Muhtasari
  • Mke na watoto wawili wa Gavana wa Wajir Mohammed Abdi hawatatoa ushahidi katika kesi ya mashtaka dhidi yake

Mke na watoto wawili wa Gavana wa Wajir Mohammed Abdi hawatatoa ushahidi katika kesi ya mashtaka dhidi yake.

Kamati ya Seneti inayosikiza kesi hiyo Jumatano ilitupilia mbali ombi hilo na bunge la kaunti ikisema hakuna sababu za kutosha za kuwalazimisha kujitokeza.

Hata hivyo, jopo hilo limeruhusu na baadaye kumwita mfanyabiashara anayedaiwa kudhibiti zabuni katika kaunti hiyo.

Bunge la kaunti, kupitia kwa wakili wake kiongozi Ahmednasir Abdullahi alikuwa ameiandikia kamati kuwaita wanne watoe ushahidi dhidi ya gavana.

Hao ni Khaire Omar Maalim, mke wa gavana, mtoto wake Yussuf Mohamed Abdi na binti Farhiya Mohamed Abdi.

Waombaji pia walitaka kuitwa kwa Osman Abdi Jimale, mfanyabiashara.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Okongo Omogeni hata hivyo alisema kuwa wawakilishi wadi wako huru kutoa na kujenga kesi yao kuonyesha kwamba familia ya gavana ilikuwa na uhusiano na makosa katika kaunti hiyo.