SIASA ZA BBI

Atwoli atishia kumtia mbaroni Cyprian Nyakundi

Nyakundi alidai kuwa Atwoli alikuwa akitarajia nafasi kuu serikalini baada ya BBI kupitishwa

Muhtasari

•Nyakundi alimuita Atwoli mwizi na mlaghai

•Atwoli amekuwa katika mstari wa mbele kupigia debe BBI

atwoli
atwoli

Katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli ametishia kumpeleka kotini mwanablogu Cyprian Nyakundi na kumuagiza atafute kazi aache kuwa mvivu.

Tishio hili limetokana na ujumbe ambao Nyakundi alichapisha siku ya Jumamosi akidai kuwa bwana Atwoli alikuwa na matumaini makubwa kuwa angepata kazi katika cheo cha juu zaidi nchini baada ya kupitisha mchakato wa BBI.

Kwenye ujumbe huo, Nyakundi alidai kuwa Atwoli alikuwa ameenda likizo kwenye makazi  yake yaliyo Namanga baada ya kupora muungano wa COTU huku akimuita mlaghai na mwizi.

Akijibu ujumbe huo, Atwoli ambaye alionekana kashikwa na hasira alimwambia Nyakundi kuwa hatasita kumfanya atiwe mbaroni tena.

“Niko na kazi, sitafuti kazi nyingine. Umetiwa mbaroni hapo awali kwa kuchapisha madai yasiyo ya kweli kunihusu na nitafanya ukamatwe tena ili udhibitishe madai yako,” Atwoli alimwandikia Nyakundi.

Bosi huyo wa COTU amekuwa kwenye mstari wa mbele katika kupigia debe mchakato wa BBI. Atwoli walionekana kukutana na kiongozi wa ODM Raila Odinga na naibu kiongozi wa chama cha Jubilee David Murathe baada ya mahakama kuu kutupilia mbali mchakato wa BBI.

Ingawa mada ya mkutano huo haijawekwa wazi, inashukiwa kuwa walikuwa wanajadili mipango ya namna wangesonga mbele na mchakato huo.

Mwanasheria mkuu wa serikali Bw Kihara Kariuki ametoa ilani ya kata rufaa maamuzi ya mahakama kuu kutupilia mbali mchakato wa BBI. Viongozi wanaoupigia debe mchakato huo wameendelea kusuta maamuzi ya koti.