Kenya na Tanzania zatia saini makubaliano ya kuondoa vikwazo mipakani

Muhtasari
  • Kenya na Tanzania zatia saini makubaliano ya kuondoa vikwazo mipakani
  • Kuwezesha upitishaji wa bidhaa mpakani hususani vinjwaji baridi kama juisi kutoka Tanzania kwenda Kenya

Tanzania na Kenya zimetia saini makubaliano ya kuondoa vikwazo vya kibiashara ambavyo vilikuwa vikizuia ushirikiano mzuri wa kufanya biashara.

Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania, Profesa Kitila Mkumbo alisema kuwa utiaji wa makubaliano hayo ni mojawapo ya jitihada za kuwezesha mahusiano ya biashara na nchi jirani kufuatia ziara iliyofanywa nchini Kenya

Alisema jumla ya vikwazo 37 vilijadiliwa katika mkutano wa pande zote hapo awali na kati ya hivyo vikwazo 19 viliondolewa na pande zote mbili zilikubaliana na kuweka mpango maalumu wa kutatua masuala yaliyobaki

Katika mkutano wa tano walijadili masuala ya kibiashara katika sekta za kilimo, forodha, uhamiaji na usafirishaji ambapo masuala 30 kati ya 64 na mengine yaliyobaki yamewekewa mkakati maalumu na muda wa utekelezaji.

Miongoni mwa masuala makuu manne waliyotatua upande wa Tanzania ni:

Kuwezesha upitishaji wa bidhaa mpakani hususani vinjwaji baridi kama juisi kutoka Tanzania kwenda Kenya.

Kuondolewa kwa tozo za ukaguzi zilizokuwa zinatozwa na mamlaka ya Kenya kwenye bidhaa za Tanzania ikiwemo unga wa ngano wenye alama ya ubora kutoka mamlaka husika Tanzania.

Kuwezesha upitishaji wa mahindi kutoka Tanzania kwenda KenyaKuondoa ushuru wa asilimia 25 kwenye bidhaa za kioo kutoka Tanzania kwenda Kenya.

Waziri alisema kwa upande wa Kenya, mambo ambayo wameweza kukubaliana ni pamoja na kutoa upendeleo kwa bidhaa za saruji zinazozalishwa nchini Kenya ambazo zinakidhi matakwa ya vigezo vya uasili wa bidhaa za jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alisema kuwa jambo lingine ni kutoa upendeleo maalumu kwa vinywaji kutoka Kenya ikiwemo juisi za nanasi baada ya kukidhi vigezo vya bidhaa vya jumuiya ya Afrika Mashariki.

Jambo lingine ni kuhakikisha bidhaa zinazoharibika haraka kama vile maziwa zinapewa kipaumbele zinapovuka mipaka kutoka Kenya kuingia Tanzania kwa kuzingatia taratibu za sheria ya forodha, huku jambo lingine likiwa ni kuongeza muda wa kibali cha kuingiza bidhaa za mifugo kutoka siku 15 hadi siku 30.

Kwa upande wake Waziri wa Kenya wa Viwanda na Biashara Betty Maina amesema hatua hiyo ni nzuri ili kuimarisha biashara kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi wa Tanzania na Kenya.