Mwangi amkejeli Atwoli kwa kuajiri 'wahuni' kulinda ishara ya barabara

Mwanaharakati Boniface Mwangi alikuwa ameapa kuwa angeangusha ishara ya 'Francis Atwol Road' iwapo angeipata bado imesimama atakaporudi

Muhtasari

• Mwangi alikuwa ameenda nchini Luxembourg kupokea tuzo la mpatanishi bora wa vijana(Outstanding Peace Maker) kwenye hafla ya Luxembourg Peace Prize

• Alipewa motisha wa kuangusha ishara hiyo na wanamitandao wengi ikiwemo wakili Ahmednassir Abdullahi aliyemuahidi kumuwakilisha mahakamani iwapo angeshikwa.

Mwanaharakati Boniface Mwangi alipoenda kuona ishara ya Francis Atwoli Road siku ya Jumatano
Mwanaharakati Boniface Mwangi alipoenda kuona ishara ya Francis Atwoli Road siku ya Jumatano
Image: Twitter

Mwaharakati Boniface Mwangi amemkejeli  katibu mkuu wa COTU, Francis Atwoli kwa kuajiri walinzi watatu kulinda ishara ya barabara ya ‘Francis Atwoli Road”

Siku  ya Jumatano, mwanaharakati huyo alitangaza kuwa alikuwa amerudi nchini na kuelekea mtaani Kileleshwa ili kuangusha ishara ya barabara ile kama alivyoahidi ila akagundua kuwa kulikuwa na watu watatu wanalinda ishara ile.

“Nimerudi, nilienda kuangalia ishara haramu ya Dik Dik Road. Inachakesha kuona kuwa Atwoli ameajiri wahuni watatu kulinda ishara ile. Atwoli anastawi kwa vurugu na vitisho ili mambo yake yafanikishwe. Tutazuia makabiliano ila  lazima ishara hiyo ianguke” Mwangi aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Siku ya Jumapili, mwanaharakati huyo ambaye alikuwa ameenda nchini Luxembourg kupokea tuzo la mpatanishi bora wa vijana(Outstanding Peace Maker) kwenye hafla ya Luxembourg Peace Prize aliapa kuwa angeangusha ishara hiyo iwapo ataipata imesimama bado wakati atarudi.

Alipewa motisha wa kuangusha ishara hiyo na wanamitandao wengi ikiwemo wakili Ahmednassir Abdullahi aliyemuahidi kumuwakilisha mahakamani iwapo angeshikwa.

Asubuhi ya siku ya Alhamisi, Mwangi aliagiza Wakenya wapatane katika eneo la Dik Dik mida ya saa saba mchana.