Rais Kenyatta aonya viongozi wanaoeneza chuki baina ya jamii

Rais alisema kuwa kuna baadhi ya viongozi wanaotumia jina la Alshabaab kueneza chuki na uhasama wa kijamii.

Muhtasari

•Rais alisisitiza kuwa usalama wa nchi ni jukumu la kila mtu huku akiagiza yeyote aliye na silaha haramu kusalimisha kwa maafisa wa  kulinda usalama.kupitia mpango wa msamaha wa serikali

Rais Uhuru Kenyatta amewaonya viongozi ambao wanaeneza uhasama baina ya jamii kisha kulaumu wanamgambo wa Al-shabaab.

Alipokuwa anaongea siku ya Jumatano katika kituo cha mafunzo ya wanapolisi cha Ngong, rais alisema kuwa serikali imetia juhudi kupigana na Alshabaab ila kunao baadhi ya viongozi ambao wanatumia jina la Alshabaab kueneza chuki na uhasama wa kijamii.

‘’Tunatazamia kupigana na tumeweza kupigana na Alshabaab. Ila hatutakubali viongozi na watu binafsi kutumia jina la Alshabaab kuendelezaa chuki na uhasama wa kijamii” Rais alisema.

Rais pia alizungumzia umuhimu wa kusuluhisa migogoro kupitia njia ya mazungumzo huku akisema kuwa serikali ikotayari kushirikiana na Wakenya katika kusuluhisha migogoro kwa njia za amani.

“Nchi ya Kenya yaweza kuwa na umoja tukikubali kushirikiana na kusuluhisha mashida zetu kwa njia ya  mazungumzo. Serikali iko tayari kushirikiana na Wakenya wote katika mambo kama hayo” Kenyatta alisema.

Rais alisisitiza kuwa usalama wa nchi ni jukumu la kila mtu huku akiagiza yeyote aliye na silaha haramu kusalimisha kwa maafisa wa  kulinda usalama kupitia mpango wa msamaha wa serikali . Aliwaonya watakaokosa kusalimisha silaha hizo kuwa watachukuliwa hatu kali za kisheria.

“Silaha haramu inashusha usalama wako bali sio kukulinda. Silaha haramu inakufanya kuwa mharifu na unahatarisha kupatana na mkono wa sheria” Rais alisema.

Siku ya Jumatano Rais aliongoza shughuli ya kuchoma silaha haramu 5,144 na silaha mzee za serikali  katika kituo cha mafunzo ya polisi cha Ngong, kaunti ya Kajiado.

Alisihi wanaotengeneza silaha haramu manyumbani kujiunga na kiwanda cha kutengeneza silaha cha Ruiru.