Raia wa Uganda azuiliwa kwa mauaji ya ajuza, 81

Mwili wa Ngina ulipatikana na rafiki yake, Salome Njambi, ukiwa umetupwa kwenye zizi la ng’ombe katika kijiji cha Karambaini pande za Limuru.

Muhtasari

•Kulingana na naibu kamanda maeneo ya Limuru, Gitonga Thumi, mwili wa marehemu ulikuwa na ishara ya mapambano kabla ya kifo chake kuashiria kuwa Ngina alijaribu kupigana na muuaji wake.

•Wakaziwa kijiji cha Karambaini wameeleza kuwa mshukiwa huyo ambaye ni raia wa Uganda hana marafiki wowote katika kijiji hicho.

Marehemu Margaret Ngina
Marehemu Margaret Ngina
Image: The Star

Mlinzi wa shamba raia wa Uganda anazuiliwa katika kituo cha  Polisi cha Tigoni kama mshukiwa kwenye mauaji ya muajiri wake mwenye umri wa miaka 81.

Jamaa huyo anashukiwa kuhusika  katika mauaji ya Margaret Ngina aliyepatiana akiwa ameuliwa siku ya Jumatano.

Mwili wa Ngina ulipatikana na rafiki yake, Salome Njambi, ukiwa umetupwa kwenye zizi la ng’ombe katika kijiji cha Karambaini eneo la  Limuru.

Njambi alipata mwili huo wakati alifika kumtembelea. Inadaiwa kuwa  alifuata mlio wa simu ya marehemu hadi kwenye zizi la ng’ombe baada ya kumkosa rafikiye kwa nyumba yake na kuamua kumpigia kujua aliko.

Kilichopata macho yake kilimpelekea kupiga nduru ambayo iliwaita majirani.

Kulingana na naibu kamanda wa polisi eneo la Limuru, Gitonga Thumi, mwili wa marehemu ulikuwa na ishara ya mvutano kabla ya kifo chake kuashiria kuwa Ngina alijaribu kupigana na muuaji wake.

Thumi alisema kuwa wapelelezi kutoka kituo cha Tigoni wameanza upelelezi huku mfanyikazi wake akizuiliwa.

“Mwanamke huyo anaishi na mtunza shamba wake. Ingawa hatuwezi zungumzia mengi kuhusu upelelezi tuliofanya, tumemzuilia mtunza shamba huyo kama mshukiwa ili atusaidie kwa upelelezi” Thumi alisema.

Wapelelezi katika boma ya Margaret Ngina
Wapelelezi katika boma ya Margaret Ngina
Image: George Mugo

Wakazi wa kijiji cha Karambaini wameeleza kuwa mshukiwa huyo ambaye ni raia wa Uganda hana marafiki wowote katika kijiji hicho.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Tigoni. Uchunguzi wa maiti utafanywa ili kusaidia katika upelelezi.

(Nhariri: Davis Ojiambo)