Rais wetu ametekwa nyara! Kuria asema rais amekuwa meneja wa NASA

Amemtaka rais kujiuzulu na kuwachia naibu wake, William Ruto kiti cha urais kwani amejiunga na upinzani.

Muhtasari

•“Nataka kuwaambia watu haswa wa eneo la Mt. Kenya ambalo mimi mwenyewe natoka, mko peke yenu. Rais wetu amechukuliwa, rais wetu ametekwa nyara,rais wetu amevamiwa na magaidi, rais wetu ametuwacha, hatuna baba hatuna mama, sisi ni mayatima, tuko peke yetu. Kwa hivyo tuanze kujipanga” Kuria alisema.

Mbunge wa Gatunndu Kusini, Moses Kuria
Moses Kuria Mbunge wa Gatunndu Kusini, Moses Kuria

Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria amekashifu tamko la rais kuwa ataunga mkono atakayeteuliwa kuongoza muungano wa NASA iwapo viongozi wa mrengo huo  wataungana na kuamua nani atapeperusha bendera.

Kuria amedai kuwa rais Uhuru Kenyatta amegura serikali na kujiunga na upinzani na kusema kuwa ni haki yake binafsi kuunga mkono mtu yeyote ampendae.

Akizungumza siku ya Jumanne, Kuria ameeleza Wakenya kuwa wako kivyao kwa sasa kwani rais Kenyatta alikuwa amewatelekeza.

“Amevuka kutoka serikalini  na kuunga mkono upinzani. Sijui kama amewacha ofisi yake wazi vile miaka kumi na tatu liyopita ofisi ya upinzani ikiwa wazi na kuingia serikalini” Kuria alisema huku akitoa mfano wa mwaka wa 2007  ambapo rais aligura upinzani na kujiunga na serikali ya rais Mwai Kibaki.

Kuria alidai kuwa rais Kenyatta amekuwa mwanaharakati na meneja wa kampeni wa mrengo wa NASA.

“Ametuwacha kwa mataa, amewacha serikali, amewacha majukumu ambayo tulimchagua aendeleze na amekuwa meneja wa kampeni na mwanaharakati wa chama cha NASA” Kuria aliendelea kusema.

Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa naibu rais William Ruto amemtaka rais kujiuzulu na kuwachia Ruto kiti cha urais kwani amejiunga na upinzani.

Kuria alimkashifu rais kwa kutohusisha wabunge wa Jubilee kwenye maswala yanahusiana na uongozi wa nchi. Amesema kuwa rais Kenyatta hajawahi waalika mkutano kuwaeleza kuhusiana na salamu za ‘handshake’ wala mchakato wa BBI.

Ningependa kumwambia rais Uhuru Kenyatta, wakati mlisalimiana na mheshimiwa Raila Odinga, aliita wabunge wa chama chake akawaelezea kiini na maana ya salamu. Sisi katika Jubilee rais hajatuita hata siku moja kama wabunge wa Jubilee atuelezee maana ya salamu, atuelezee mambo ya BBI, atuambie tuchukue msimamo upi kwa BBI. Lakini anaendelea kukutana na wabunge na viongozi kuzingatia misingi ya kikabila” Kuria alisema.

Kutokana na madai hayo, Kuria amesema kuwa rais ndiye tishio kubwa la umoja wa kitaifa huku akidai kuwa anaendeleza sera za kikabila.

Alikuwa anatoa hisia hizo kufuatia mkutano kati ya rais na viongozi kutoka Ukambani ambao ulifanyika siku ya Jumatatu.

Kwenye mkutano huo, rais aliwasihi viongozi kushirikiana pamoja huku akiapa kuunga mkono atakayeteuliwa kuongoza mrengo wa NASA iwapo viongozi hao wataungana.

Kuria ameshauri Wakenya haswa wakazi wa eneo la Mt. Kenya kujipanga kwa madai kuwa rais alikuwa amewatekeleza.

“Nataka kuwaambia watu haswa wa eneo la Mt. Kenya ambalo mimi mwenyewe natoka, mko peke yenu. Rais wetu amechukuliwa, rais wetu ametekwa nyara,rais wetu amevamiwa na magaidi, rais wetu ametuwacha, hatuna baba hatuna mama, sisi ni mayatima, tuko peke yetu. Kwa hivyo tuanze kujipanga” Kuria alisema.

Matamshi hayo ya Kuria yanawiana na ujumbe ambao naibu rais alichapisha kwenye mitandao ya Twitter na Facebook siku ya Jumanne alikosoa tamko la rais kuhusiana na chaguo la mridhi wa kiti chake.

Ruto alisema kuwa angejipanga na usaidizi wa Mungu kuona kuwa rais hakuwa tayari kumuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu mwaka ujao.