Waiguru akemea Kimunya kwa kutishia wakazi wa Kiambaa

Gavana Waiguru amedai kuwa rais Kenyatta amepeleka maendeleo mpaka maeneo ya watu ambao hawakumpigia kura akipeana mfano na Kisumu.

Muhtasari

•Kimunya alitisshia wakazi wa Kiambaa kuwa iwapo hawatamchagua mgombeaji wa Jubilee hawatapata usaidizi kutoka kwa serikali.

•Waiguru ametenganisha chama cha Jubilee na maoni ya Kimunya huku akisema kuwa rais hana ubaguzi kwa wale ambao hawakumchagua.

Gavana Waiguru akizungumza mwakani 2019
Gavana Waiguru akizungumza mwakani 2019
Image: Hisani

Gavana wa kaunti ya Kirinyaga Anne Waiguru amepuuzilia mbali tamko la kiongozi wa wengi bungeni, Amos Kimunya kuwa serikali haitatenga pesa kwa eneo bunge la Kiambaa iwapo hawatachagua mgombeaji kiti hicho na tikiti ya Jubilee.

Waiguru ametenganisha chama cha Jubilee na maoni ya Kimunya huku akisema kuwa rais hana ubaguzi kwa wale ambao hawakumchagua.

"Tumeskia maneno ambayo yametoka  kwamba kuna mmoja wetu ambaye alitishia watu wa Kiambaa akawaambia kuwa wasipochaguana  hawatapata usaidizi kutoka kwa serikali. Mimi kama mmoja wa chama cha Jubilee nataka kujitenga na kutenganisha chama chetu na maoni hayo. Sisi tuko katika serikali na serikali ya Jubilee inayoongozwa na rais Uhuru Kenyatta haitenganishi Mkenya mmoja na mwingine" Waiguru alisema.

Alikuwa akihutubia wanahabari baada ya mkutano na gavana wa Machakos Alfred Mutua ambaye alikuwa amemtembelea katika makazi yake upande wa Kagio, kaunti yake ya Kirinyaga siku ya Jumanne.

"Nataka kuomba watu wa Kiambaa wasisikize propaganda na uvumi ambao unatoka kwa watu ambao hawataki kusaidia rais ama kusaidia chama chetu cha Jubilee. Sisi tunaunganisha Wakenya wote na tumeshirikiana na vyama vyote" Waiguru aliendelea kusema

Gavana huyo alidai kuwa rais Kenyatta amepeleka maendeleo mpaka maeneo ya watu ambao hawakumpigia kura akipeana mfano na Kisumu.

Alisisistiza kuwa Wakenya wana haki ya kufanya maamuzi binafsi bila ya kutishiwa na yeyote. Hata hivyo, aliwaomba wakazi wa Kiambaa kumpigia kura Kariri Njama ambaye anapeperusha bendera ya Jubilee kwenye uchaguzi mdogo eneo hilo ambao utafanyika tarehe 15 mwezi ujao.

"Ujumbe wangu kwa watu wa Kiambaa ni, chagueni Jubilee kwa sababu Jubilee ndicho chama kitakacholeta maendeleo" Waiguru alisema.

Siku ya Jumamosi, Mbunge wa Kipipiri Amos Kimunya alirekodiwa akitishia waumini katika kanisa moja upande wa Kiambaa kuwa iwapo hawatamchagua mgombeaji wa Jubilee hawatapata usaidizi  kutoka kwa serikali.

"Watu wa Kiambaa kama hamtanipatia Kariri Njama, nitawaangazia kweli? Hata mabilioni hayo ya pesa mnaahidiwa kwa barabara, sio nyinyi pekee mnazihitaji. Ikiwa mtachagua mtu ambaye hatafanya kazi na serikali, hata zenyewe hazitapatikana. " Kimunya alisema

Viongozi wengi haswa wandani wa naibu rais wameendelea kumkashifu Kimunya kufuatia matamshi hayo.