Polisi waonywa dhidi ya kutangaza malalamiko yao kwenye mitandao

Maafisa watakaopatikana na makosa ya kuelezea malalamishi yao kupitia mitandao au wanahabari watachukuliwa hatua.

Muhtasari

•Mutyambai alisema kuwa ni hatia kwa wanapolisi kutoa habari yoyote inayohusiana na mambo ya wanapolisi bila  kupewa mamlaka ya kufanya hivo.

•Haya yanajiri siku chache tu baada ya afisa mmoja mwanamke upande wa Mombasa kusimulia masaibu yake kupitia video iliyoenezwa kwenye mitandao ya kijamii.

Mutyambai
IG Hillary Mutyambai Mutyambai

Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai amewaonya maafisa wa polisi dhidi ya kueleza malalamiko yao kupitia mitandao ya kijamii.

Kupitia ujumbe uliandikiwa wakuu wa polisi siku ya Alhamisi, Mutyambai ameeleza kuwa visa vya maafisa wa polisi kueleza kutoridhika kwao kupitia mitandao ya kijamii vimeongezeka. 

Mutyambai amewataka maafisa hao kutumia njia zote rasmi  kabla ya kuchukua hatua kama zile.

Kulingana na ujumbe huo ambao ulikuwa umetiwa saini na mkurugenzi wa DCI, Mwangi Wanderi, maafisa watakaopatikana na makosa ya kuelezea malalamishi yao kupitia mitandao au wanahabari watachukuliwa hatua.

Mutyambai alisema kuwa ni hatia kwa wanapolisi kutoa habari yoyote inayohusiana na mambo ya wanapolisi bila  kupewa mamlaka ya kufanya hivo.

"Sheria inakataza maafisa wa polisi kupitisha ujumbe kutumia mitandao ya kijamii isipokuwa ni utekelezaji wa kazi rasmi" Mutyambai alisema.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya afisa mmoja mwanamke upande wa Mombasa kusimulia masaibu yake kupitia video iliyoenezwa kwenye mitandao ya kijamii.

Kwenye video hiyo iliyoenezwa sana mitandaoni mwezi uliopita, afisa yule alikuwa anaomba Mutyambai kukubali ombi lake la kuacha kazi  huku akidai kuwa alikuwa amemuandikia barua nyingi ila hazikumfikia.

"Nataka tu nijiuzulu kwa amani. Nimeandika barua nyingi kwa Inspekta Generali ila hazimfikii. Ndio maana maafisa wengi wanafadhaika hadi kujitia kitanzi. Mimi sitaki kujiua" Afisa yule alisema.

Afisa huyo alilalamikia unyanyasaji wa kimapenzi, ufisadi na dhuluma kwenye idara ya polisi. Alieleza kuwa alitaka kuwacha kazi ya polisi akitaja kuwa anaweza kustawi mahala pengine