Vijana wa 'ghetto' wachanga pesa kuweka upya ishara ya 'Francis Atwoli Road'

Kikundi hicho kinapendekeza barabara ya Jogoo Road ibadilishwe jina iitwe Atwoli Road

Muhtasari

•Vijana hao ambao walikuwa wametoka   mitaa mbalimbali jijini Nairobi walidai kuwa mapenzi yao kwa katibu mkuu wa COTU yaliwafanya kuchanga pesa za kutengeneza ishara hiyo.

•Kikundi hicho kiliendelea kupendekeza barabara ya Jogoo Road ibadilishwe jina iwe Atwoli Road kwa madai kuwa ile iiyokuwa Dik Dik Road ni ndogo sana. Walipendekeza barabara zingine kubadilishwa majina na kupewa ya viongozi wengine mashuhuri nchini.

Ishara ya barabara ya Francis Atwoli Road yawekwa upya
Ishara ya barabara ya Francis Atwoli Road yawekwa upya
Image: Hisani

Ishara ya barabara ya 'Francis  Atwoli Road' imeendelea kuibua gumzo kubwa baina ya Wakenya na kukabiliwa na utata mwingi.

Hapo awali, ishara hiyo imewekwa tena mara mbili baada ya kuangushwa na kuchomwa na watu wasiojulikana.

Siku ya Jumanne, Kikundi cha vijana kiliandamana hadi maeneo yale huku kikiwa kimebeba ishara iliyopambwa na kuandikwa 'Francis Atwoli Road' na kubadilisha ishara iliyokuwa imewekwa tena baada ya kuchomwa wiki iliyopita.

Vijana hao ambao walikuwa wametoka   mitaa mbalimbali jijini Nairobi walidai kuwa mapenzi yao kwa katibu mkuu wa COTU yaliwafanya kuchanga pesa za kutengeneza ishara hiyo.

"Tumekuja kuonyesha Atwoli upendo kwa sababu yeye ni mwanaghetto mwenzetu. Atwoli ni mtu wa kwanza kufaulu kutoka ghetto kwa hivyo tunamuona yeye kama mfano mzuri kwetu.Kwa kuwa tumeona kuna wakora wanamnyanyasa ndio maana tumechanga pesa na tukakuja kuweka ishara yetu" Mmoja wa vijana hao alisema.

Kikundi hicho kiliendelea kupendekeza barabara ya Jogoo Road ibadilishwe jina iwe Atwoli Road kwa madai kuwa ile iiyokuwa Dik Dik Road ni ndogo sana. Walipendekeza barabara zingine kubadilishwa majina na kupewa ya viongozi wengine mashuhuri nchini.

Vijana hao walionya mwanaharakati Boniface Mwangi na mwanablogu Robert Alai dhidi ya kile walisema ni kunyanyasa Atwoli na kueneza maneno ya chuki na uongo dhidi yake.

Usiku wa kuamkia Jumanne wiki iliyopita ishara ya barabara hiyo ilichomwa na watu wasiojulikana na kuwekwa tena baadae siku hiyo. Ishara hiyo ilioakwa rangi upya na maadishi ya 'Francis Atwoli Road' kuandikwa tena.

Vijana walioweka ishara mpya wameapa kuilinda dhidi ya wahalifu.