Sossion ajiuzulu wadhifa wa katibu mkuu wa Knut

Kiongozi huyo akihutubia mkao wa wanahabari alisema siku ya Ijumaa "amezidi kiwango cha kuwasilisha matakwa ya wafanyikazi kupitia Knut

Muhtasari

• Katibu Mkuu wa chama cha kutetea maslahi ya walimu nchini Knut Wilson Sossion amejiuzulu.

• Sossion alijiuzulu siku ya Ijumaa baada ya miaka mitatu ya mzozo wa uongozi katika muungano huo.

Katibu mkuu wa KNUT Wilson Sossion

Katibu mkuu wa muungano wa kitaifa wa Walimu (Knut) Wilson Sossion amejiuzulu wadhifa huo.

Sossion alijiuzulu siku ya Ijumaa baada ya miaka mitatu ya mzozo wa uongozi katika muungano huo.

Kiongozi huyo akihutubia mkao wa wanahabari alisema siku ya Ijumaa "amezidi kiwango cha kuwasilisha matakwa ya wafanyikazi kupitia Knut," na ataangazia kutetea wafanyikazi kupitia wadhifa wake akiwa mbunge katika bunge la kitaifa.

Kujiuzulu kwa Sossion kunajiri siku moja tu kabla ya uchaguzi wa kitaifa wa viongozi wa muungano huo uliopangwa kufanyika Jumamosi katika Uwanja wa Michezo wa Ruaraka jijini Nairobi.

Ametimiza miaka tisa ya utumishi katika uongozi wa muungano wa Knut, kwanza akihudumu kama mwenyekiti kabla ya kuchukua jukumu kubwa la Katibu Mkuu ambaye pia ndiye msemaji wa muungano huo.

Sossion katika hotuba yake ya kujiuzulu alisema kwamba alikuwa tayari kufungua njia ikiwa hatua hiyo itaruhusu Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) kurejelea kuwasilisha makato ya walimu kwa muungano huo.

Wakati wa tangazo lake la kujiuzulu, Sossion alisifu mafanikio yake wakati akihudumu katika Knut.

"Nitabaki mwaminifu kwa Knut na nitapatikana kila wakati kushauri na kuunga mkono uongozi mpya," alisema.

Katibu Mkuu wa Muungano wa KNUT Wilson Sossion
Katibu Mkuu wa Muungano wa KNUT Wilson Sossion

Sossion alisema wanachama wa Knut wanastahili kupongezwa kwa uvumilivu wao licha ya kufadhaishwa na serikali.

Uchaguzi uliopangwa kufanyika kesho ulikuwa umewagawanya vikali maafisa wakuu wa Knut huku mrengo mmoja ukiimarissha juhudi za kumng’oa Sossion.

Wanamlaumu kwa masaibu ambayo yameukumba muungano huo katika miaka mitatu iliyopita. Chini ya uongozi wake uanachama wa Knut ulipungua kutoka kiwango cha juu kabisa cha 187,000 hadi 16,000.

Uteuzi wa Sossion na Chama cha ODM kuwa mbunge maalum pia ulizua utata, na TSC na hata kupelekea kuondolewa kwa jina lake kutoka sajili ya TSC.