Mwanamke afungwa miaka 7 kwa jaribio la kuua mpenzi wake wa mwezi mmoja kwa kutumia kisu

Khalea alisema kuwa alikuwa ametoka kukunywa tembo na pamoja na wanaume fulani na aliporudi akapata Ngure akiwa amefunga mlango kutoka ndani.

Muhtasari

•Ebby Khalea alipatiwa hukumu hiyo na hakimu mkuu katika mahakama ya Kibera baada ya kesi dhidi yake kuthibitishwa.

•Mzozo ulipokuwa unaendelea, Ngure alisikika mwenye uchungu huku akiomba usaidizi kutoka kwa majirani.

•Majirani walipofika pale walipata kisu iliyojawa na damu kwenye sakafu huku Ngure akiwa ameshika Khalea akimuuliza mbona alikuwa amemdunga. Ngure alipelekwa katika hospitali ya Mama Lucy kwa bodaboda.

court
court

Mwanamke mmoja kutoka eneo la Embakasi amehukumiwa kifungo cha miaka 7 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya jaribio la kuua mpenzi wake.

Ebby Khalea alipatiwa hukumu hiyo na hakimu mkuu katika mahakama ya Kibera baada ya kesi dhidi yake kuthibitishwa.

Inadaiwa kuwa Khabea alimdunga mpenzi wake wa mwezi mmoja, Michael Ngure akiwa nyumbani kwake maeneo ya Kisumu Ndogo mnamo Julai 31.

Shahidi mmoja alisema kuwa Khalea alikuwa ametoka kupiga maji na kupata Ngure akiwa amelala huku amefunga mlango kutoka ndani.

Hapo akaamua kuomba panga kutoka kwa jirani ili afungue mlango kwa kusukuma msumari uliokuwa umefunga.

Baada ya mlango kufunguka, jirani alichukua upanga wake na kuenda kulala.

Baadae aliamshwa na vurugu zilizokuwa zinaendelea kwa nyumba ya Ngure. Wapenzi wale wawili walikuwa wakizozana.

Mzozo ulipokuwa unaendelea, Ngure alisikika mwenye uchungu huku akiomba usaidizi kutoka kwa majirani.

Majirani walipofika pale walipata kisu iliyojawa na damu kwenye sakafu huku Ngure akiwa ameshika Khalea akimuuliza mbona alikuwa amemdunga. Ngure alipelekwa katika hospitali ya Mama Lucy kwa bodaboda.

Pale hospitalini alifanyiwa upasuaji na kulazwa siku kadhaa kabla ya polisi kuanza kushughulikia ile kesi.

Maafisa wa polisi na wapelelezi walifika katika eneo la tukio na kisu ambacho kilitumika kutekeleza uvamizi ule kikapatikana.

Daktari alithibitisha kuwa madhara ambayo yalisababishwa kwenye mwili wa Ngure yalikuwa mabaya. Hata hivyo, Khalea alikanusha kuwa alimdunga mpenzi wake ambaye walikuwa wamechumbiana kwa kipindi cha mwezi mmoja tu.

Khalea alisema kuwa alikuwa ametoka kukunywa tembo na pamoja na wanaume fulani na aliporudi akapata Ngure akiwa amefunga mlango kutoka ndani. Hapo akaomba jirani panga afungue mlango na akaingia. Baadae wakawa na mzozo.

Alisema kuwa walipigania kisu ile na Ngure akadungwa katika harakati zile.

Hata hivyo, mahakama ilimpata na makosa baada ya kuangazia ushahidi ambao ulitolewa. Khalea atakula kalenda kwa kipindi cha miaka saba.