KILIO CHA HAKI

Jamaa aliyekatwa uume wake na makahaba Kakamega atafuta haki

Alisema kuwa alivamiwa na wafanyakazi wa ngono zaidi ya 10 kwa madai kuwa alikataa kulipa baada ya kuhudumiwa na mmoja wao

Muhtasari

•SA, 27, alisema kuwa alivamiwa na wafanyakazi wa ngono zaidi ya 10  mjini Kakamega mwezi Juni mwaka uliopita.

•"Nilipomwambia kuwa nililipia huduma zake, akanipiga kofi na wengine wakatokea na kumsaidia kunipiga. Walinipiga kisha wakakata uume wangu ambao walirusha kwenye barabara na wakaenda" Aliendelea kusimulia.

black-woman-crying-
black-woman-crying-

Habari na Hilton Otenyo.

Mwanaume aliyepoteza uume wake baada ya kuzozana na kahaba mmoja mjini Kakamega mwaka uliopita ametoa ombi kwa mashirika ya kutetea haki za binadamu kumsaidia kupata haki.

SA, 27, alisema kuwa alivamiwa na wafanyakazi wa ngono zaidi ya 10  mjini Kakamega mwezi Juni mwaka uliopita.

Alisema kuwa walimpiga kabla ya kukata uume wake kwa madai kuwa alikataa kulipa baada ya kuhudumiwa na mmoja wao.

"Nilipatana na mwanamke huyo na tukakubaliana kuwa ningemlipa shilingi 150 kwa huduma fupi na nikamlipa mbele ya kuanza shughuli. Tuliingia chumbani na ni kama kulikuwa na mwanamke mwingine chini ya kitanda kwani nilipomaliza na kuamka kuchukua suruali yangu, kibeti changu hakikuwepo"

Nilipomuuliza mahali kibeti changu kingeweza kuwa kimeenda, akawa mkali na akaanza kunipiga huku anapiga nduru. Wengine wakaja na kumsaidia kunipiga" mwanaume huyo alielezea The Star siku ya Jumatano.

Alisema kuwa baada ya kupokea kichapo walimfurusha nje na akaenda nyumbani.

Mwanaume huyo alieleza kuwa  mwanadada yule alikabiliana naye barabarani siku iliyofuata na akadai malipo.

"Nilipomwambia kuwa nililipia huduma zake, akanipiga kofi na wengine wakatokea na kumsaidia kunipiga. Walinipiga kisha wakakata uume wangu ambao walirusha kwenye barabara na wakaenda" Aliendelea kusimulia.

Alisema kuwa baada ya hayo alishuhudia maumivu makali hadi akapoteza fahamu. Fahamu yake ilirejea akiwa hospitalini.

Alisema kuwa kahaba yule alipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Kakamega kuwa alikuwa amekataa kulipia huduma alizopewa. Alikamatwa akiwa hospitalini na kufikishwa mahakamani. Alisema kuwa mwenye kumushtaki hakuwahi fika mahakamani tangu mwezi Juni mwaka uliopita na kupelekea kufutitiliwa mbali kwa mashtaka hayo mnamo Juni 3 mwaka huu.

Hata hivyo, The Star haingeweza kuthibitisha mashtaka aliyokabiliwa nayo mahakamani kwani hangeweza kukumbuka nambari ya kesi hiyo. Juhudi za kupata rekodi za jela ya Kakamega pia ziliangulia patupu.

Polisi upande wa Kakamega walisema kuwa hakuwahi piga ripoti kuhusu mashambulio hayo

Mwanaume huyo anaomba mashirika ya kutetea haki za binadamu kuingilia kati na kumsaidia kupata haki yake.