Kenya yakanusha kuhusika na kukamatwa kwa mwanaharakati wa Nigeria, Nnamdi Kanu

Balozi Machage amewataka wanaotoa tuhuma hizo kutoa pia na ushahidi.

Muhtasari

•Balozi wa Kenya, nchini Nigeria, Wilfred Machage amewaambia waandishi wa habari kwamba tuhuma kuwa Kenya imehusika katika kukamatwa kwake ‘ni za kutungwa, kufikirika na za kuungwaungwa’

•Serikali ya Nigeria imesema Kanu alikamatwa jumapili lakini haikusema alikamatiwa wapi na kwa namna gani, huku Balozi Machage akisema Kenya haina mpango wa kuingilia masuala ya ndani ya Nigeri

wilfred machage
wilfred machage
Image: Hisani

Siku mbili baada ya Uingereza kukanusha kuhusika katika kukamatwa na kurudishwa kwa Nnamdi Kanu, mwanaharakati anayeongoza kundi la Biafra linalotaka kujitenga kwa jimbo la kusini-mashariki mwa Nigeria, Kenya nayo imekanusha.

Balozi wa Kenya, nchini Nigeria, Wilfred Machage amewaambia waandishi wa habari kwamba tuhuma kuwa Kenya imehusika katika kukamatwa kwake ‘ni za kutungwa, kufikirika na za kuungwaungwa’

Balozi Machage amewataka wanaotoa tuhuma hizo kutoa pia na ushahidi. Alikuwa akijibu tuhuma kwamba Nnamdi alikamatwa kwenye nchi hiyo ya Afrika Mashariki. Kaka yake na Nnamdi Kanu, ainukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba kaka yake alikamatiwa Kenya.

Serikali ya Nigeria imesema Kanu alikamatwa jumapili lakini haikusema alikamatiwa wapi na kwa namna gani, huku Balozi Machage akisema Kenya haina mpango wa kuingilia masuala ya ndani ya Nigeria

Kanu ambaye kundi lake linadaiwa ni la kigaidi na kupigwa marufuku na Serikali ya Nigeria, alitoroka nchini humo mwaka 2017 akikabiliwa na shitaka la jinai ya uhaini.

Serikali ya Uingereza ilitoa taarifa wiki hii ikisema kuwa inatambua kukamatwa kwakwe lakini inathibitisha kwamba hajakamatiwa nchini Uingereza.

Mwaka 2009 Kanu (53) alianzisha redio Biafra na kurusha matangazo Nigeria kutokea London, akitumia njia hiyo kudai uhuru wa Biafra na kuwataka wafuasi wake kubeba silaha dhidi ya taifa la Nigeria.

Kanu ambaye kesi yake inatarajiwa kusikilizwa Julai 26 mwaka huu, aliwahi kukamatwa mwaka 2015 na kuzua maandamano makubwa nchini humo.