Mudavadi akosoa hatua ya serikali kutoza ushuru bidhaa muhimu

Amesema kuwa hili ni pigo kuu kwa wakenya hasa wakati huu mgumu

Muhtasari

•Wakenya  sasa watagharamika kulipa shilingi 350 zaidi wanaponunua gesi kufuatia ushuru wa 16% ambao utatozwa bidhaa hiyo.

•Awali alikutana na Gavana wa kaunti ya Nakuru Lee Kinyanjui ambapo walizungumza kwa kina uwezekano wa kunasua wakenya kutoka kwa hali ngumu ya kimaisha. 

Musalia Mudavadi akisalimia wakazi wa Nakuru siku ya Jumamosi, Julai 3
Twitter//Musalia Mudavadi Musalia Mudavadi akisalimia wakazi wa Nakuru siku ya Jumamosi, Julai 3

Kinara wa Chama cha  Amani National Congress(ANC) Musalia Mudavadi ameikosoa serikali kwa  hatua ya kuongezwa kwa ushuru kwenye bidhaa muhimu hasa zinazotumika kwa matumizi ya kila siku.

Akigusia ongezeko kwenye bei ya gesi kutokana na ushuru wa juu utakaotozwa, Mudavadi amesema kuwa hili ni pigo kuu kwa wakenya hasa wakati huu mgumu ambapo uchumi wa taifa upo kwenye hali mbovu na mapato ni ya chini mno.

"Ushuru kwa gesi unamfuata mwanamke hadi jikoni, anatarajiwa kufanya nini? Si atakata miti ili apata kuni ama makaa?" Mudavadi alisema.

 Mudavadi amesema kuwa hili ni pigo kuu kwa wakenya hasa wakati huu mgumu ambapo uchumi wa taifa upo kwenye hali mbovu na mapato ni ya chini mno.

Mudavadi alihutubia wanahabari akiwa Nyayo Garderns, kaunti ya Nakuru ambako ako katika ziara ya siku mbili eneo hilo.

Awali alikutana na Gavana wa kaunti ya Nakuru Lee Kinyanjui ambapo walizungumza kwa kina uwezekano wa kunasua wakenya kutoka kwa hali ngumu ya kimaisha. 

Alimpongeza gavana Kinyajui, uongozi wa kaunti hiyo na wakazi wa  huko kwa kuinuliwa hadhi kwa mji wa Nakuru kuwa jiji.

Mudavadi ambaye ashatangaza azma yake ya kuwania Urais pia amewaomba wakenya kumpa nafasi ya kuliongoza taifa huku akiahidi kupunguza ushuru, ufisadi na deni la kitaifa iwapo watamkabidhi kiti cha urais.

Alitaja kuwa ataangazia  kuboresha uchumi ili wakenya wote wafaidike na pia kupunguza mzigo wa madeni ya umma kutokana na mikopo mikubwa ili kutoa nafasi za kubuni ajira hasa kwa vijana.