Kinara wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka amewahimiza Wakenya kukumbatia mchakato wa BBI.
Akihutubia waumini katika kanisa ya Katoliki ya Kisooni, Kalonzo aliwaomba Wakenya kupitisha BBI kwani akisema kuwa italeta mageuzi nchini.
Hata hivyo, amewahakikishia wananchi kuwa hakuna yeyote atawalazimisha kupigia kura mchakato huo.
"Hakuna mtu atakuja amebeba panga ama bakora akuambie lazima hiki kwa namna yoyote. Ni mambo ya kujadiliana na mafikra. Tuwe na mashindano ya mawazo kwani hati hii ni hati ya mageuzi. Wacha tusiwe nchi pekee duniani ambayo haina mageuzi. Wazo nzuri hutengeneza nafasi kwa wazo nzuri zaidi" Kalonzo alisema.
Mwanasiasa huyo ambaye alikuwa mgombea mwenza wa kinara wa ODM, Raila Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa 2017 aliwasihi Wakenya kutopinga BBI bila sababu.
Alisema kuwa mchakato huo ni wa Wakenya wote ila sio wa rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga.
"Kuna watu ambao wanapinga jambo bila sababu yoyote. Mahakama ya kukata rufaa ikituruhusu tutarudi kueleza wananchi maana na athari ya BBI. Hii ni hoja ya kutengeneza katiba. Hii kitu ni zaidi ya Uhuru Kenyatta na Raila Odinga, ni ya Wakenya wenyewe. Ni sharti tufikirie zaidi" Kalonzo alisema.