SIASA ZA 2022

Huyu wetu hananga hangovers! Askofu Margaret Wanjiru amsifia naibu rais William Ruto

Wanjiru pia alithibitisha nia yake ya kuwania kiti cha gavana wa Nairobi kwa tikiti ya UDA.

Muhtasari

•Alimtaja naibu rais kama muumini ambaye anafuata desturi za Ukristo.

•Wanjiru pia alisisitiza nia yake ya kuwania kiti cha gavana wa Nairobi kwa tikiti ya UDA.

Askofu Margaret Wanjiru
Askofu Margaret Wanjiru
Image: Facebook// Bishop Margaret Wanjiru

Aliyekuwa mbunge wa Starehe, askofu Margaret Wanjiru ameendelea kumpigia debe naibu rais William Ruto tunapokaribia uchaguzi mkuu wa 2022.

Akihutubia waumini katika kanisa ya PCEA Umoja siku ya Jumapili, Wanjiru alisema kuwa anafurahia kumfanyia Ruto kampeni kwani yeye ni Mkristo kamili kama yeye.

Alisema kuwa naibu rais si mlevi na kwa hivyo hana shida yoyote na kufika kanisani.

"Inanifurahisha sana kuwa naweza kusimama na kuhubiri, kuwa naweza kusimama na kupiga kampeni na naibu rais kwani yeye ni Mkristo kama mimi. Kuwa haitulazimu kuenda mahali kwanza na kungoja amalize 'hangovers' ndio akuje kanisa! Hapana, huyu wetu hananga hangovers."Wanjiru aliambia waumini.

Alimtaja naibu rais kama muumini ambaye anafuata desturi za Ukristo. 

"Tunashukuru Mungu kwa maisha yake, tunamshukuru kwa familia yake, tunashukuru Mungu kwa kuwa tunaweza kuzungumzia Bibilia tunapomtumikia Mungu na Wakenya. Naibu rais tunakupenda na tunakupongeza" Wanjiru alisema.

Wanjiru pia alithibitisha nia yake ya kuwania kiti cha gavana wa Nairobi kwa tikiti ya UDA.

"Upande wa siasa, mimi mama Bishop Margaret Wanjiru nimerudi kwa uwanja ninawania kiti cha gavana wa Nairobi. Sisi kama kanisa ningependa kuwasihi tusikae mbali safari hii na siasa ya Kenya" Wanjiru alisema.

Siku ya Ijumaa, askofu Wanjiru alisisitiza kuwa ahadi ya jamii ya GEMA kwa naibu rais kuwa watamuunga mkono kwenye uchaguzi ujao bado inasimama.

"Tulisema kuwa tutaunga mkono mmoja wetu kwa kipindi cha miaka kumi, kisha tukuunge mkono kwa sababu ulituunga mkono kwa miaka kumi ijayo. Hatubadilishi. Kama kuna mmoja wetu ambaye ameamua kuwa mdanganyifu, sisi hatutavutwa kwa hayo, tutasimama na ukweli. Umekuwa hapo kuunga wengine mkono, ulimuunga Raila akawa waziri mkuu, nilikuwa kwa serikali hiyo. Uliunga mkono ndugu yangu Uhuru Kenyatta akawa rais, sasa ni wakati wetu, tutakubeba kwa mabega yetu hadi uwe rais" Wanjiru alisema.