Mkasa Watamu; Mvuvi afariki baada ya kuzama katika bahari Hindi

Serikali imeagizwa kuhakikisha wavuvi wanapata misaada ya dharura wakati wa mikasa.

Muhtasari

•Kulingana na mwenyekiti wa usimamizi wa fuo za bahari BMU eneo hlilo Athman Mwambire,marehemu kwa jina Kazungu Mwangale alikuwa na wenzake wakivua kabla ya boti lao kushindwa kuhimili mawimbi makali na kuzama.

•Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika chumba cha uhifadhi wa maiti cha Hospitali ya kaunti ndogo ya Malindi.

Indian Ocean
Indian Ocean
Image: ALPHONCE GARI

Habari na Alphonce Gari:

Mvuvi mmoja eneo la Watamu Kilifi kaskazini ameaga dunia baada ya kuzama katika bahari hindi wakati alipokuwa akiendeleza shughuli zake za uvuvi wa samaki eneo hilo.

Kulingana na mwenyekiti wa usimamizi wa fuo za bahari BMU eneo hlilo Athman Mwambire,marehemu kwa jina Kazungu Mwangale alikuwa na wenzake wakivua kabla ya boti lao kushindwa kuhimili mawimbi makali na kuzama.

Mwambire ameongeza kuwa kwenye mkasa huo,wavuvi wawili wamenusurika baada ya kufanikiwa kuogolea hadi katika fuo za bahari.

"Walikuwa wameenda  baharini usiku waliporudi wakapigwa na wimbi wakazama. Wawili wakatoka kwenye boti lakini mmoja akabaki. Kati ya wawili walioshuka mmoja akavuka mwingine akafa maji" Mwambire alisema.

Mwambire sasa ametoa tahadhari kwa wavuvi eneo hilo kuwa makini wakati huu ambapo kunashuhudiwa upepo mwingi na mawimbi makali baharini.

Aidha anaitaka serikali kuweka mikakati ya kuhakikisha wavuvi wanapata misaada ya dharura wakati wa mikasa.

"Wito wangu kwa serikali naomba kwamba ikiwezekana tuje tutolewe mlango hapa Watamu. Mlango ndio muhimu sana kwa sababu huo ndio utafanya matatizo yote yaishe. Waje wafungue katika hii  mwamba hapa watoe mlango ili mvuvi akitoka awe hana shida  ya kupigwa na mawimbi anatoka moja kwa moja" Mwambire aliomba"

Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika chumba cha uhifadhi wa maiti cha Hospitali ya kaunti ndogo ya Malindi.