Spika Justin Muturi atangaza hadharani nia ya kuwania kiti cha Urais

Muturi alisema kuwa yeye pekee ndiye ana uwezo wa kurejesha mpango na nidhamu nchini.

Muhtasari

•Akihutubia viongozi wa dini akiwa nyumbani kwake maeneo ya Mbeere Kaskazini, kaunti ya Embu ambako alikuwa amewaalika, Muturi alieleza imani yake kuwa ana uwezo wa kunyakua kiti hicho.

•Muturi alisema amehitimu kuwa rais na akapuuzilia mbali madai kuwa angekuwa mgombea mwenza wa mgombezi fulani.

Viongozi wa dini wakimuombea spika Justin Muturi akiwa nyumbani kwake Embu siku ya Jumamosi
Viongozi wa dini wakimuombea spika Justin Muturi akiwa nyumbani kwake Embu siku ya Jumamosi
Image: Benjamin Nyagah

Spika wa bunge la kitaifa, Justin Muturi ametangaza hadharani nia yake ya kuwania kiti cha urais mwaka ujao.

Akihutubia viongozi wa dini siku ya Jumamosi akiwa nyumbani kwake maeneo ya Mbeere Kaskazini, kaunti ya Embu ambako alikuwa amewaalika, Muturi alieleza imani yake kuwa ana uwezo wa kunyakua kiti hicho.

Muturi alisema kuwa yeye pekee ndiye ana uwezo wa kurejesha mpango na nidhamu nchini Kenya akiruhusiwa kuongoza.

"Ni sharti turejeshe utulivu na heshima hapa nchini na hii haiwezi katimia iwapo siko uongozini. Lazima  tuwe na taifa lenye nidhamu na mpango. Ni mimi pekee ambaye naweza fanya hayo nikiwa rais" Muturi alisema.

Muturi alisema amehitimu kuwa rais na akapuuzilia mbali madai kuwa angekuwa mgombea mwenza wa mgombezi fulani.

"Nimesema hapo awali kuwa mimi sihuhisiki kwenye kinyang'anyiro ili niwe mgombea mwenza ila nataka nichukue kiti cha juu zaidi. Najua namna nchi inaendelezwa na niko na uwezo wa kuongoza taifa kama rais" Muturi alisema.

Siku ya Ijumaa, spika Muturi alihimiza  Wakenya kumuunga mkono kwani angeleta nidhamu na uwazi katika sekta ya huduma za umma. Alisema kuwa vitendo vinavyokiuka kanuni na maadili vimezuia taifa la Kenya kutimia uwezo wake.`

"Rais Mwai Kibaki alileta mpango wa vision 2030 na Uhuru akaleta Ajenda nne kuu ila kufuatia utovu wa nidhamu mipango hiyo imekuwa ngumu kuafikiwa" Alisema.

Mwezi mmoja uliopita, Muturi alitawazwa kama msemaji wa eneo la mlima Kenya na baadhi wazee wa jamii ya GEMA.

Hafla hiyo iliibua gumzo kubwa baina ya viongozi wengine na wakazi wa wa eneo hilo wengine wakimuunga mkono huku wengine wakipinga hafla hiyo haswa wale kutoka eneo la kati.

Hata hivyo, viongozi wengi kutoka eneo la Mashariki wameendelea kuunga spika mkono na kuwaagiza viongozi wengine wa GEMA kumuunga mmoja wao mkono pia.