Suleiman Shahbal agura Jubilee na kujiunga na ODM

Muhtasari
  • Suleiman Shahbal ahama rasmi Jubilee, ajiunga na ODM
  • Katika uchaguzi mkuu wa 2017 chini ya tiketi ya Jubilee, ambako alipoteza kiti hicho kwa gavana Hassan Joho
  • Joho alijizolea kura 221,363,huku Shahbal akiwa katika nafasi ya pili na kura 69,429
Suleiman
Image: star

Mgombea kiti cha ugavana wa zamani kaunti ya Mombasa Suleiman Shahbal amejiuzulu rasmi kutoka chama tawala cha Jubilee na kujiunga na ODM.

Katika uchaguzi mkuu wa 2017 aliwania kiti cha gavana wa Mombasa kwa tiketi ya Jubilee, na kushindwa na gavana Hassan Joho.

Joho alijizolea kura 221,363, huku Shahbal akimaliza wa pili kwa kura 69,429.

Katika barua ya tarehe 6 Julai, mfanyabiashara huyo maarufu wa Mombasa alimwambia Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju kwamba alikuwa akitumia haki zake za kikatiba kuondoka chama tawala.

"Katika utekelezaji wa haki zangu za kikatiba na za kisheria kuwa kwa chama cha kisiasa ninacho pendelea  kulingana na kifungu cha 14 cha Vyama vya Kisiasa, 2011, ningependa  kujiuzulu kama mwanachama wa Jubilee," Ilisoma barua hiyo.

Kupitia akaunti yake ya Twitter, Suleiman alisema kuwa sasa anajiunga na chama cha upinzani cha ODM.

Hatua yake kujiunga na chama cha ODM kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022 inatarajiwa kuongeza joto la kisiasa katika kuanti ya Mombasa, huku muhula wa gavana wa sasa Hassan Joho ukikamilika mwaka wa 2022.

Katika mazungumzo ya simu ya awali na gazetti la the Star, Shahbal alisema kampeni za jubilee zilivurugwa na malumbano ya ndani kwa ndani ambayo yalifanya kuwa vigumu kufanikisha ajenda yao.

Mgombea mwenza wa Shahbal katika uchaguzi wa mwaka 2017 Ananiah Mwaboza alikuwa pia ameonyesha nia yake kuania kiti hicho kwa tikiti ya Jubilee lakini Naibu Rais William Ruto aliingilia kati.