Mshangao baada ya chatu kutembelea boma la 'rafikiye' marehemu na kujilaza kitandani Baringo

Inadaiwa kuwa marehemu aliwapenda nyoka sana.

Muhtasari

•Esther Ewoi ambaye  ni mjane ya marehemu alisema kuwa hawakuona haja ya kufukuza au kumuua nyoka yule kwani waliamini kuwa alikuja kuomboleza kifo cha rafiki yake.

•Kulingana na Esther, nyoka huyo alipitia penye kaburi ya marehemu kabla ya kuingia ya kuingia ndani ya nyumba, kupanda juu ya kitanda, kujiviringisha na kulala kimya kimya.

Nyoka ambaye aliingia ndani ya boma ya marehemu Nakarot
Nyoka ambaye aliingia ndani ya boma ya marehemu Nakarot
Image: JOSEPH KANGOGO

Habari na Joseph Kangogo

Hali ya mshangao ilitanda katika maeneo ya Kampi ya Samaki, Baringo siku ya Ijumaa baada ya chatu mkubwa kutembelea boma la 'rafiki' yake aliyeaga. mnamo Juni 30.

Chatu huyo aliingia ndani ya boma ya Ewoi Nakarot almaarufu kama Dr William ambaye aliaga na umri wa miaka 86 na kujilaza juu ya kitanda alichokuwa analalia.

Inadaiwa kuwa marehemu aliwapenda nyoka sana.

Esther Ewoi ambaye  ni mjane ya marehemu alisema kuwa hawakuona haja ya kufukuza au kumuua nyoka yule kwani waliamini kuwa alikuja kuomboleza kifo cha rafiki yake.

"Mume wangu alifariki mnamo Juni 30 baada ya kuugua kwa kipindi kifupi na tukamzika Alhamisi kisha nyoka yule mnyenyekevu akatutembelea Ijumaa mida ya saa tano usiku. Tuliamini kuwa aliamua kuja kutembea na kuomboleza rafiki yake marehemu" Bi Esther alisema.

Marehemu Ewoi Nakarot akionyesha ushupavu wake kabla ya kufariki
Marehemu Ewoi Nakarot akionyesha ushupavu wake kabla ya kufariki
Image: JOSEPH KANGOGO

Kulingana na Esther, nyoka huyo alipitia penye kaburi ya marehemu kabla ya kuingia ya kuingia ndani ya nyumba, kupanda juu ya kitanda, kujiviringisha na kulala kimya kimya.

"Kwetu ni baraka. Labda mume wangu aliamua kujionyesha kwetu kupitia nyoka huyo ambaye aliishi kutunza vizuri maishani mwake." Esther alisema.

Mwanawe marehemu, Vincent Ewoi alisema kuwa asubuhi iliyofuata waliarifu majirani kuhusu tukio hilo ambao walifika kujionea miujiza ile kabla yake kumkamata chatu yule kwa mikono yake na kumuachilia aende kichakani.

Vincent alisema kuwa nyoka ndio walikuwa wanaletea familia yao mapato kwani babake alikuwa akiwauza na kuwapa mafunzo ya kufuga nyoka.