Msaidizi wa gavana Obado alisaidia katika kutekwa nyara kwa Sharon Otieno -Shahidi

Inadaiwa kuwa msaidizi huyo aliwadanganya kuingia kwenye gari ambalo lilipeleka Sharon kukumbana na kifo chake

Muhtasari

•Konstabo Willy Okoti amearifu mahakama kuwa  alipokuwa katika kituo cha polisi cha Kadel mida ya saa tatu usiku wa Septemba 3, 2018, msamaria mwema alimleta shahidi ambaye kwa sasa analindwa baada yake kuweza kutoroka kutoka kwa gari ambalo walikuwa wamedanganywa kuabiri.

•Kufuatia tishio hilo mwanahabari yule akaamua kuruka kutoka kwa gari lililokuwa linaenda na akaugua majeraha kwenye magoti na kitanga cha mkono wake.

gavana obado
gavana obado
Image: Enos Teche

Habari na Susan Muhundi

Mmoja wa wasaidizi wa gavana wa Migori Okoth Obado alimdanganya Bi. Sharon Otieno na shahidi mwingine ambaye anawekewa ulinzi kuingia kwa gari ambalo lilikuwa limeegeshwa mita  300 toka hoteli moja mjini Rongo usiku wa mauaji ya mwanadada huyo.

Konstabo Willy Okoti amearifu mahakama kuwa  alipokuwa katika kituo cha polisi cha Kadel mida ya saa tatu usiku wa Septemba 3, 2018, msamaria mwema alimleta shahidi ambaye kwa sasa analindwa baada yake kuweza kutoroka kutoka kwa gari ambalo walikuwa wamedanganywa kuabiri.

Shahidi yule ambaye anadaiwa kuwa mwanahabari alimuarifu kuwa walikuwa na Sharon katika hoteli moja na msaidizi mmoja wa Obado alikuwepo pia.

Ingawa mwanahabari huyo hakutaja jina la msaidizi huyo, alisema kuwa aliwaomba kuingia kwenye gari waelekee katika hoteli nyingine.

Wawili hao waliingia kwenye gari kisha likaendeshwa kuelekea Homabaya. 

Walipokuwa ndani ya gari , mwanahabari yule alianza kutishiwa kuuawa kwa kuhusika katika uchunguzi wa madai kuwa gavana Obado alimpachika mimba mwanadada huyo, shahidi alisema.

Kufuatia tishio hilo mwanahabari yule akaamua kuruka kutoka kwa gari lililokuwa linaenda na akaugua majeraha kwenye magoti na kitanga cha mkono wake.

Sharon mwenyewe alibaki kwenye gari na mwili wake ukapatikana baadae ukiwa umelala juu ya dimbwi la damu  katika kichaka cha Kodera maeneo ya Oyugi's.

Okoti alieleza kuwa shahidi alikuwa akitetemeka kwa uwoga wakati alikuwa anasimulia yaliyokuwa yametokea