'Wakati wa siasa chafu umwekwisha!' Mudavadi akosoa wanasiasa wanaohadaa Wakenya kwa kuwapa hongo

Mudavadi amesisitiza kuwa ufufuaji wa uchumi na kubuni ajira kwa vijana ndilo lengo lake kuu

Muhtasari

• Musalia Mudavadi amewataka wakenya kuweka kwenye mizani sera na agenda zitakazokuwa zikipigiwa uungwaji mkono na wagombeaji mbali mbali wa nyadhifa za uongozi wa kisiasa kwenye kura ya mwaka 2022.

•Amepuuzilia mbali siasa za mrengo wa upinzani wa NASA na kusema kuwa Imani ya wafuasi wa NASA imedidimia pakubwa na kwake anasaka kufufua Imani hiyo na mwanzo mpya. 

Kinara wa ANC Musalia Mudavadi. Picha:HISANI
Kinara wa ANC Musalia Mudavadi. Picha:HISANI

Kinara wa chama cha ANC Musalia Mudavadi amewataka wakenya kuweka kwenye mizani sera na agenda zitakazokuwa zikipigiwa uungwaji mkono na wagombeaji mbali mbali wa nyadhifa za uongozi wa kisiasa kwenye kura ya mwaka 2022.

Akiwa Nyeri alipomtembelea Gavana wa Kaunti ya Nyeri Mutahi Kahiga Mudavadi amesisitiza kuwa ufufuaji wa uchumi na kubuni ajira kwa vijana ndilo lengo lake kuu kwenye kusaka kura za wakenya za Urais ifikiapo debe la mwaka 2022.

Amewakososa viongozi wanaowahadaa wananchi na hasa vijana kwa kuwapa hongo na kiinua mgongo huku wakidai kuwa wao ndio watakaofufua uchumi wa taifa la Kenya.

Mudavadi akisema kuwa wakati wa siasa chafu umekwisha na sasa ni sharti wakenya wazinduke na kufahamu kuwa sera bora ndizo ambazo zitalikomboa taifa hili.

Mudavadi alitumia fursa hii kutilia shime suala la uaminifu kwenye miungano na kusema kuwa chama cha ANC kinasaka marafiki waaminifu ambao wataketi kwenye meza ya mazungumzo na yale watakayoafikiana yasiwe tu kwenye wino wa karatasi bali yawe yale watakayoyatenda kwa vitendo kwa minajili ya kuwapa wakenya mwamko mpya.

Amepuuzilia mbali siasa za mrengo wa upinzani wa NASA na kusema kuwa Imani ya wafuasi wa NASA imedidimia pakubwa na kwake anasaka kufufua Imani hiyo na mwanzo mpya.

Baadaye alikutana na wadau mbali mbali na kusemezana nao ana kwa ana na Hapo kesho atahudhuria Ibaada kadhaa za jumapili Nyeri na pia kukutana na wananchi wa tabaka mbali mbali ili kukuza azma ya safari yake ya Ikulu.

Alikuwa amaendamana na viongozi kadhaa wa ANC kutoka mlima Kenya Pamoja na wabunge Sakwa Bunyasi na Beatrice Adagala na Mwenyekiti wa ANC Kelvin Lunani.