IEBC yakanusha madai ya DCI kuwa mitambo ya kuhifadhi data za wapiga kura ilidukuliwa

Kulingana na Chebukati, mitambo ya BVR haijawahi kudukuliwa na yeyote tangu kuwekwa na kuzinduliwa kwake miaka minane iliyopita kwani haijaunganishwa na mtandao.

Muhtasari

•Siku ya Jumamosi, maafisa wa DCI walikuwa wamedai kuwa kikundi cha walaghai wa kimitandao kilidukua mitambo ya IEBC na kupata maelezo ya watu 61,617 kutoka kaunti moja maeneo ya Magharibi mwa Kenya wakiwa na njama ya kuwalaghai kimitandao

•Chebukati alisema kuwa huenda genge lililonaswa na DCI lilipata maelezo yale kihalali kutoka kwa tume kupitia maombi rasmi na baada ya kulipa kiwango fulani kinachohitajika.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati

Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini (IEBC) imepinga madai kuwa mitambo inayotumika kuhifadhi data za wapiga kura ilidukuliwa na maelezo ya wapiga kura 61,617 yakaibiwa.

Siku ya Jumamosi, maafisa wa DCI walikuwa wamedai kuwa kikundi cha walaghai wa kimitandao kilidukua mitambo ya IEBC na kupata maelezo ya watu 61,617 kutoka kaunti moja maeneo ya Magharibi mwa Kenya wakiwa na njama ya kuwalaghai kimitandao.

Ujumbe uliotolewa na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebutai jioni ya  Jumapili ulipuuzilia mbali madai hayo.

Kulingana na Chebukati, mitambo ya BVR haijawahi kudukuliwa na yeyote tangu kuwekwa na kuzinduliwa kwake miaka minane iliyopita kwani haijaunganishwa na mtandao.

"Mitambo ya BVR ambayo inatumika kuhifadhi data za wapiga kura imeundwa kwa namna kuwa iinatumia mtandao wake wa  kipekee, eti ya servers ili kuhakikisha uaminifu, usiri na upatikanaji wa hali ya juu. Tangu kuwekwa na kuzinduliwa kwake miaka minane iliyopita kwani haijaunganishwa na mtandao" Chebukati alidai.

Bosi wa IEBC alisema kuwa mitambo ya tume hiyo iko chini ya ulinzi wa hali ya juu.

Chebukati alisema kuwa huenda genge lililonaswa na DCI lilipata maelezo yale kihalali kutoka kwa tume kupitia maombi rasmi na baada ya kulipa kiwango fulani kinachohitajika.

Genge  hilo liliripotiwa kutumia maelezo ambayo walipata kwenye mitambo ya IEBC  kuwatapeli  maajenti wa huduma mbalimbali za simu wakidai kuwa wamiliki rasmi wa simu fulani ili kuweza kupata kibali cha kutumia akaunti za kimitandao za wahasiriwa.