Mshangao Bungoma baada ya jamaa kuchimba kaburi lake na kutishia kujitoa uhai ili kuepuka deni la 15,000

Martin Juma, 46, alipoulizwa kwa nini akaamua kuchukua hatua hiyo alidai kuwa alikuwa na deni ya watu kadhaa kijijini ambao walikuwa wanamlazimisha kulipa.

Muhtasari

•Bibiye Juma alithibitisha uwepo wa deni la 15,000 na kusema kuwa bwanake alikuwa ameshindwa kulipa kwa kuwa hana kazi.

•Mzee mmoja wa kijiji, Kizito Lukorito, alidai kuwa kulingana na mila na desturi za jamii ya Waluhya iwapo mtu atapatikana akichimbua kaburi lake anafaa kupigwa vibaya na kondoo mweusi kuchinjwa ili kufukuza pepo mbaya kabla ya shina la ndizi kuzikwa pale.

Martin Juma atazama kaburi alilopatikana akijichimbia
Martin Juma atazama kaburi alilopatikana akijichimbia
Image: ROSELAND LUMWAMU

Habari na Roseland Lumwamu

Mwanaume mmoja katika kijiji cha Namakhele maeneo ya Kabuchai, Bungoma amewashtua wanakijiji baada yake kuchimbua kaburi lake mwenyewe akitishia kujitoa uhai ili kuepuka kulipa deni la shilingi 15,000.

Martin Juma, 46, alipoulizwa kwa nini akaamua kuchukua hatua hiyo alidai kuwa alikuwa na deni ya watu kadhaa kijijini ambao walikuwa wanamlazimisha kulipa.

Kuona kuwa hana kazi ya kumletea mapato aweze kulipa madeni yake Juma alionelea heri atayarishe kaburi lake kisha ajitoe uhai.

Bibiye Juma alithibitisha uwepo wa deni la 15,000 na kusema kuwa bwanake alikuwa ameshindwa kulipa kwa kuwa hana kazi.

Mzee mmoja wa kijiji, Kizito Lukorito, alidai kuwa kulingana na mila na desturi za jamii ya Waluhya iwapo mtu atapatikana akichimbua kaburi lake anafaa kupigwa vibaya na kondoo mweusi kuchinjwa ili kufukuza pepo mbaya kabla ya shina la ndizi kuzikwa pale.

Lukoririto alisema kuwa iwapo tendo hilo la kidesturi halitafanyika basi huenda familia ya mhusika ikapoteza mmoja wao.