"Mbona ilikuchukua muda mrefu hivo Baba?" Moses Kuria apongeza Raila kwa kugura NASA

Kulingana na Kuria, kinara wa ODM amekuwa akibeba wanasiasa wengine mgongoni kwa kipindi kirefu ila kama punda shukurani zao zimekuwa mateke tu.

Muhtasari

•Kuria alitumia ukurasa wake wa Facebook kumpongeza Odinga baada ya chama chake cha ODM kutangaza kujiondoa rasmi kutoka muungano wa ODM siku ya Alhamisi.

•Katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna alitoa tangazo la kujiondoa kwa ODM siku ya Alhamisi na kudai kuwa wangeandikia msajili wa vyama vya kisiasa kuhusu uamuzi huo.

Image: HISANI

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria amempongeza aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga kwa hatua ya kujitenga na muungano wa NASA.

Kuria alitumia ukurasa wake wa Facebook kumpongeza Odinga baada ya chama chake cha ODM kutangaza kujiondoa rasmi kutoka muungano wa ODM siku ya Alhamisi.

Kulingana na Kuria, kinara wa ODM amekuwa akibeba wanasiasa wengine mgongoni kwa kipindi kirefu ila kama punda shukurani zao zimekuwa mateke tu.

"Huo ndio uamuzi wa busara ambao rafiki yangu baba amefanya, kujiondoa kutoka muungano wa NASA. Unabeba watu mgongoni. Wanajifaidi na kura zako, nguvu zako na pesa. Wanakukwaruza hingo. Wanakukojolea na kisha wanasema kuwa wao ndio wanafaa kuwania urais eti wewe hauwezi chaguliwa." Kuria alisema.

Kuria alisema kuwa kiongozi wa ODM alikuwa amechelewa kufanya uamuzi huo.

"Mbona ukachukua muda mrefu hivo Baba" Aliuliza Kuria.

Katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna alitoa tangazo la kujiondoa kwa ODM siku ya Alhamisi na kudai kuwa wangeandikia msajili wa vyama vya kisiasa kuhusu uamuzi huo.

Sifuna alisema kuwa chama hicho kiko kwenye harakati ya kuunda ushirikiano na vyama vingine.

"Tunakadiria kuanzisha mpango wa kuunda ushirikiano mpya na kuendeleza majadiliano na washirika wetu wapya," Sifuna alisema.

Alisema kuwa mikutano ya maeneo mepangwa tayari kwa ushirikiano na vyama ambavyo vina maono sawa  na ya ODM.