Msichana wa miaka 10 anayedaiwa kunajisiwa na mjomba wake mara nyingi tangu 2019 afariki, Baringo

Maumivu yalishinikiza msichana huyo kutoroka nyumbani kwa shangazi yake miezi miwili iliyopita na kuishi kichakani kwa kipindi cha takriban wiki moja akila matunda ya kichaka.

Muhtasari

•Msichana huyo wa miaka 10 anaripotiwa kufariki mnamo Julai 24 kutokana na majeraha akiwa katika nyumba ya watotot ya Sunrise iliyo maeneo ya Kabarnet.

•Alisema kuwa mjomba wake alimtishia kumuua iwapo angethubutu kuambia yeyote kuhusu yaliyokuwa yakiendelea.

Mshukiwa Haron Cherono anayedaiwa kubaka mpwa wake tangu 2019
Mshukiwa Haron Cherono anayedaiwa kubaka mpwa wake tangu 2019
Image: JOSEPH KANGOGO

Msichana wa darasa la tatu kutoka kaunti ya Baringo  anayesemekana kunajisiwa na mjomba wake kwa miaka mitatu tangu mwaka wa 2019 ameaga dunia.

Msichana huyo wa miaka 10 anaripotiwa kufariki mnamo Julai 24 kutokana na majeraha akiwa katika nyumba ya watoto ya Sunrise iliyo maeneo ya Kabarnet.

Mjomba wake Haron Cherono anayetuhumiwa kumnajisi hajulikani aliko.

Mnamo Ijumaa msimamizi wa nyumba ya watoto ya Sunrise, Titus Barmasa alisema kuwa waligundua kuwa afya ya msichana huyo haikuwa nzuri wakati aliletwa katika kituo hicho miezi miwili iliyopita.

Alisema kuwa familia ya mtoto huyo haikuwapatia ripoti yake ya kidaktari ambayo ingewasaidia kufanya mipango ya matibabu maalum.

Barmasai alisema kuwa mida ya usiku wa manane msichana huyo aliomba mtu mmoja kushika tumbo lake na akaomba kuletewa maji, maembe na soda kabla yake kuzirai na kufariki.

Inadaiwa kuwa kufikia kifo chake  kichwa, uso na viungo vyake vingine vilikuwa vimefura.

Msichana huyo anaripotiwa kunajisiwa na mjomba wake Haron Cherono, 60, mara nyingi  akiwa nyumbani kwao maeneo ya Baringo Kaskazini.

"Mjomba wangu angenivuruta kila jioni mwendo wa saa moja hadi saa mbili na kunipeleka katika chumba chake cha malazi wakati shangazi yangu bado alikuwa dukani" Msichana huyo alisema.

Alisema kuwa mjomba wake alimtishia kumuua iwapo angethubutu kuambia yeyote kuhusu yaliyokuwa yakiendelea.

"Hangejali hata nikipiga nduru vipi ama kuvunja damu" Alisema.

Maumivu yalishinikiza msichana huyo kutoroka nyumbani kwa shangazi yake miezi miwili iliyopita  na kuishi kichakani  kwa kipindi cha takriban wiki moja akila matunda ya kichaka.

Wanakijiji waliokuwa wanamtafuta walimpata akiwa dhaifu na mwenye njaa.

Vipimo vya kidaktari katika hospitali ya Moi Teaching and Referral mnamo Juni 14 viliashiria kuwa nyumba ya mtoto, figo na maini ya marehemu yalikuwa yameharibika.

OCPD wa Baringo Kaskazini Fredrick Odinga alisema kuwa mshukiwa bado hajulikani aliko ila wanaendelea kumtafuta.

Mkewe mshukiwa anazuiliwa na atafikishwa mahakamani siku ya Jumatatu.

(Utafsiri; Samuel Maina)