Ruto adai kuwa utawala wa Uhuru umevuruga uchumi

Muhtasari

• Uhusiano kati ya Uhuru na Ruto unazidi kuzorota.

• Ruto alisema uchumi umeharibiwa, mamilioni ya watu wameachwa kwenye lindi la ufukara na deni la umma ambalo limetimia kiawango cha kutamausha

Naibu William Ruto
Image: Douglas Okiddy

 TAARIFA YA JULIUS OTIENO NA GIDEON KETER

Naibu Rais William Ruto amepuuzilia mbali rekodi ya Rais Uhuru Kenyatta na kumshtumu rais wake kwa kuharibu uchumi wa nchi miongoni mwa makosa mengine mengi.

Mbali na kuongoza mikakati ya kuunda muungano mkubwa, kuna fununu kwamba Rais huenda akatangaza mabadiliko makubwa katika serikali  ili kuwafurusha washirika wa Ruto na kuunda "serikali upya".

Matamshi ya naibu rais yanajiri wakati duru zimearifu kuwa Uhuru alikuwa anapanga kufanya mkutano wa faragha na Raila mjini Mombasa.

Raila alisafiri kwenda Mombasa Jumatano jioni bila mtu yeyote. Anatarajiwa kusalia Mombasa hadi Jumapili, hatua iliyopelekea kubatilishwa kwa ratiba ya mikutano yake.

Uhusiano kati ya Uhuru na Ruto unazidi kuzorota.

Jumatatu, Ruto alizuiwa kusafiri kwenda Uganda. DP alidai kuwa tukio hilo ni moja wapo wa mipango ya kumdhalilisha.

Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Lakini akizungumza nyumbani kwake Karen baada ya mkutano na wandani wake, Ruto alisema utawala wa Uhuru uliacha ajenda zake muhimu, na kuingiza nchi katika "hali mbaya".

Ruto alisema uchumi umeharibiwa, mamilioni ya watu wameachwa kwenye lindi la ufukara na deni la umma ambalo limetimia kiawango cha kutamausha lililokusanywa baada ya Jubilee kuacha ahadi zake kwa Wakenya.

"Kwa miaka minne iliyopita, mara kwa mara tumekuwa tukiuliza maswali kuhusu hatua ya Jubilee kuachana na ajenda na ahadi zake mwaka 2017," wandani wa Ruto walisema katika taarifa ya pamoja ya vyombo vya habari.

Taarifa hiyo ilisomwa kwa zamu na wabunge ambao walitangaza rasmi kuhamia UDA – chombo ambacho naibu rais anatarajia kutumia kwa safari yake ya Ikulu.

Ruto alisema Rais na kikosi cha Upinzani walijishughulisha na BBI, na hivyo kuhujumu mipango muhimu ya Jubilee ambayo ingegeuza maisha ya Wakenya wa kawaida.

"Muungano wa Nasa, wakuu wake na washirika wao wa Jubilee waliteka nyara serikali, ajenda yake na kuhujumu kubuniwa kwa ajira, huduma za afya kwa wote, usalama wa chakula na viwanda na hivyo kukwamisha mpango mzima wa Big Four," Ruto na wenzake walisema.

Timu ya UDA pia ilidai kwamba utawala wa Uhuru uliharamisha shughuli na biashara za 'hustler' katika maeneo kama Nyamakima, Gikomba, Kamukunji, Barabara ya Kirinyaga na Barabara ya River jijini Nairobi, na kulaani wengi kwa umaskini.

Jubilee pia imesimamia kufurushwa kikatili na kinyama na ubomoaji dhidi ya wanyonge na uharibifu wa mali za kibinafsi, katika maeneo ya Kariobangi na Ruai jijini Nairobi.

"Wamesimamia vibaya uchumi na kusababisha kuongezeka marudufu kwa deni la umma," DP alisema.

Katika muhula wao wa kwanza, Ruto alitetea kila mara hamu ya serikali ya Jubilee kukopa na hata kushambulia upinzani kwa kukosoa hamu ya serikali kukopa zaidi.