Wanamitandao wajumuika kushinikiza haki itendeke kufuatia kifo cha ndugu wawili Embu

Baadhi ya wanamiandao wametumia talanta na sanaa zao kudai haki ya ndugu hao ipatikane.

Muhtasari

•Benson Njiru (22) na Emmanuel Mutura (19) ambao walikuwa wanafunzi katika chuo kikuu cha Kabarak na chuo cha mafunzo ya kiteknolojia cha Don Bosco mtawalia wanadaiwa kutoweka baada ya kukamatwa na polisi kutoka kituo cha polisi cha Manyatta mnamo Julai 1.

•Juhudi za kuwatafuta zilinoga kwa kipindi cha siku tatu zilizofuata hadi miili yao ikapatikana katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Embu  Level 5 mnamo Jumanne wiki iliyopita.

•Wanamitandao waliojawa na ghadhabu kufuatia kukithiri kwa ripoti za matendo ya kikatili miongoni mwa maafisa wa usalama wameungana na familia ya marehemu kwenye vita ya kutafuta haki.

Mandugu wawili wanaodaiwa kufariki mikononi mwa maafisa wa polisi
Mandugu wawili wanaodaiwa kufariki mikononi mwa maafisa wa polisi
Image: HISANI

Maelfu ya Wakenya mitandaoni wamejumuika kudai haki kutendeka kufuatia kifo cha ndugu wawili kutoka maeneo ya Kianjokoma, Embu.

Benson Njiru (22) na Emmanuel Mutura (19) ambao walikuwa wanafunzi katika chuo kikuu cha Kabarak na chuo cha mafunzo ya kiteknolojia cha Don Bosco mtawalia wanadaiwa kutoweka baada ya kukamatwa na polisi kutoka kituo cha polisi cha Manyatta mnamo Julai 1.

Baada ya kukamatwa kwao haikujulikana walikokuwa  na familia ikaanza juhudi za kuwatafuta.

Juhudi za kuwatafuta zilinoga kwa kipindi cha siku tatu zilizofuata hadi miili yao ikapatikana katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Embu  Level 5 mnamo Jumanne wiki iliyopita.

Familia, marafiki na  majirani wa ndugu hao wawili wameendelea kunyooshea maafisa wa polisi kidole cha lawama kufuatia kifo chao.

Wanamitandao waliojawa na ghadhabu kufuatia kukithiri kwa ripoti za matendo ya kikatili miongoni mwa maafisa wa usalama wameungana na familia ya marehemu kwenye vita ya kutafuta haki.

Chini ya alama ya reli #JusticeForKianjokomaBrothers kwenye mtandao wa Twitter, Wakenya wameendelea kushinikiza maafisa wa DCI kufanya upelelezi kuhusiana na tukio hilo kwa dharura na hatua kali kuchukuliwa dhidi ya wahusika.

Wanamitandao wengi wamelalamikia kulegea kwa wapelelezi katika uchunguzi wa tukio hilo na wameendelea kudai uchunguzi ukamilike haraka. Baadhi ya wanamiandao wametumia talanta na sanaa zao kudai haki ya ndugu hao ipatikane.

Hizi hapa baadhi ya jumbe za Wakenya;

Mnamo Ijumaa wiki iliyopita naibu inspekta Jenerali wa polisi Edward Mbugua aliagiza kuhamishwa kwa OCS wa kituo cha polisi cha Manyatta Abdullahi Yaya na OCPD wa Embu Kaskazini Emily Ngaruiya huku uchunguzi zaidi ukiendelea.

Wakuu katika idara ya polisi wakiongozwa na Mbugua walikutana na wakazi wa Embu ambao walikuwa katika siku ya tatu ya maandamano wakilalamikia mauaji ya ndugu hao wawili.