Itakuwa ngumu kutetea kiti changu na tiketi ya Jubilee - Gavana Waiguru

Waiguru amesema kuwa chama cha Jubilee kina kazi kubwa ya kufanya ili kujiimarisha tena

Muhtasari

•Alisema kuwa iwapo angeamua kugombea kiti na tiketi ya Jubilee na mwingine awanie na tiketi ya chama kingine ingekuwa ngumu kushawishi watu wampigie kura hata kama wanahisi amefanya kazi.

•Mwanasiasa huyo amedai kuwa chama cha Jubilee bado kina nafasi ya kujikomboa ila kazi kubwa sana inahitajika kufanyika.

•Hata hivyo, Waiguru alisita kuzungumzia suala la iwapo anaweza kujiunga na chama cha naibu rais cha UDA.

Gavana wa Kirinyaga Anne Mumbi
Gavana wa Kirinyaga Anne Mumbi
Image: MAKTABA

Gavana wa Kirinyaga Anne Mumbi Waiguru amesema ingekuwa ngumu sana kutetea kiti chake na tiketi ya Jubilee iwapo uchaguzi ungefanyika leo.

Akizungumza katika stesheni ya Citizen TV asubuhi ya Jumatano, Waiguru amesema kuwa chama cha Jubilee kina  kazi kubwa ya kufanya ili kujiimarisha tena.

"Ukweli ni kuwa kutetea kiti changu iwapo uchaguzi ungefanyika leo ingekuwa jambo ngumu. Huo ndio ukweli isipokuwa mabadiliko yafanyike kwenye chama cha Jubilee" Waiguru alisema.

Alisema kuwa iwapo angeamua kugombea kiti na tiketi ya Jubilee na mwingine awanie na tiketi ya chama kingine ingekuwa ngumu kushawishi watu wampigie kura hata kama wanahisi amefanya kazi.

Gavana huyo alisema kuwa chama cha Jubilee kinafaa kurejesha uhusiano mzuri na watu wa Mlima Kenya kabla ya muda kuyoyoma.

'"Jubilee inafaa kujichunguza kwa undani ili iweze kukubalika tena katika eneo la Mlima Kenya. Jubillee inafaa kutia bidii katika kujirekebisha kwa dharura. Kuimarisha chama, kuskiza watu na kurejesha chama kwa watu" Waiguru alisema.

Mwanasiasa huyo amedai kuwa chama cha Jubilee bado kina nafasi ya kujikomboa ila kazi kubwa sana inahitajika kufanyika.

Amesema kuwa hatua ya rais na naibu wake kutofanya kazi pamoja ni ya kusikitisha.

"Tunahitaji kuangazi kilichofanyika ili tusijipate katika hali ile tena kwani inatudhuru sote. Kuna kazi kubwa kuendeleza serikali na wanapokosa kufanya kazi pamoja tunafaa kujua vile tutatatua hayo" Alisema gavana huyo.

Hata hivyo, Waiguru alisita kuzungumzia suala la iwapo anaweza kujiunga na chama cha naibu rais cha UDA.

(Utafsiri: Samuel Maina)