Seneta Omanga apuuzilia mbali madai kuwa alionekana akiruka juu ya uzio wa kituo cha polisi cha Kasarani

Muhtasari

•Picha ambayo inaonyesha mwanake mwenye umbo kama wa seneta Omanga ilisambazwa sana mitandaoni siku ya Alhamisi ikidaiwa kuwa ni yeye  alionekana akiruka juu ya uzio wa kituo cha polisi cha Kasarani.

•Omanga amedai kuwa haiwezekani akaruka juu ya kitu chochote bila kusababisha mtetemeko wa ardhi nchini

Image: HISANI

Seneta wa kuteuliwa Millicent Omanga amepuuzilia mbali madai kuwa ni yeye aliye kwenye picha inayoenezwa sana mitandaoni ikionyesha mwanamke akiruka juu ya uzio.

Picha ambayo inaonyesha mwanake mwenye umbo kama wa seneta Omanga ilisambazwa sana mitandaoni siku ya Alhamisi ikidaiwa kuwa ni yeye  alionekana akiruka juu ya uzio wa kituo cha polisi cha Kasarani.

Wanamitandao walimtaka mwandani huyo wa naibu rais William Ruto kufafanua zaidi kuhusu picha ile huku madai yakiibuka  kuwa alikuwa amefika katika kituo cha Kasarani siku ya Jumatano.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo amejitokeza na kujitenga mbali na picha hiyo akidai kuwa madai hayo ni uvumi tu.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Omanga amedai kuwa haiwezekani akaruka juu ya kitu chochote bila kusababisha mtetemeko wa ardhi nchini.

"Puuzilieni mbali hiyo propaganda kuwa niliruka uzio wa kituo cha polisi cha Kasarani. Huo ni uvumi ambao haufai kuangaziwa. Kwa kweli nawezaje kuruka juu ya chochote bila Kenya kupatwa na mtetemeko wa ardhi?" Omanga aliandika kwenye mtandao wa Twitter siku ya Alhamisi.