Hofu Nyamira baada ya mwili uliokatakatwa viungo, bila kichwa kutupwa barabarani

Gunia zile zilkuwa na mifuko ya plastiki ambayo ilikuwa imewekwa viungo tofauti vya mwili wa mtu mzima ila kichwa kilikosekana.

Muhtasari

•Vipande vya mwili ule ambao ulitupwa mida ya saa nne usiku wa Jumatatu vilikuwa vimewekwa kwa gunia mbili ila kichwa hakikuwepo.

•Mashahidi walisema kwamba gari ambalo lilitumika na walioacha kama wametupa mwili huo halikuwa na nambari ya usajili.

Umati wa wakazi wa Nyamira wajumuika kuona mwili uliotupwa barabarani
Umati wa wakazi wa Nyamira wajumuika kuona mwili uliotupwa barabarani
Image: ALVIN RATEMO

Habari na Alvin Ratemo

Hali ya hofu ilitanda katika eneo la Konate kaunti ya Nyamira baada ya mwili wa mwanaume ambao ulikuwa umekatakatwa viungo kutupwa kutoka kwa gari lililokuwa linaenda kwa mwendo wa kasi.

Vipande vya mwili ule ambao ulitupwa mida ya saa nne usiku wa Jumatatu vilikuwa vimewekwa kwa gunia mbili ila kichwa hakikuwepo.

Mashahidi walisema kwamba gari ambalo lilitumika na walioacha kama wametupa mwili huo halikuwa na nambari ya usajili.

Polisi walisema kwamba gunia zile zilkuwa na mifuko ya plastiki ambayo ilikuwa imewekwa viungo tofauti vya mwili wa mtu mzima ila kichwa kilikosekana.

Mwili huo ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Nyamira County Referral.

Kamanda wa polisi katika eneo la Nyamira Kusini Moses Kirong alisema  kwamba wanafanya uchunguzi kupata ufunuo wa mauaji yale.

Kupitia kwa kurasa zake za mitandao ya kijamii, kamishna wa kaunti ya Nyamira Amos Mariba alisema kwamba maafisa wa DCI ndio walikuwa wanahusika na upelelezi wa tukio hilo.

Aliahidi uchunguzi wa haraka na kuhakikishia wakazi kwamba wataweza kunasa waliotekeleza unyama huo.