Isaac Mwaura asaidia mwanafunzi bora aliyehitaji msaada kujiunga na chuo kikuu kusoma sheria

Muhtasari

•Caroline Wanjugu Mwangi 17, alifanya mtihani wa KCSE 2020 katika shule ya upili ya wasichana ya Mahiga na kuzoa alama ya A- (pointi 78) ila familia yake haikuwa na uwezo wa kifedha wa kumpeleka katika chuo kikuu kusomea sheria.

Image: FACEBOOK// ISAAC MWAURA

Seneta aliyebanduliwa Isaac Mwaura amesaidia msichana aliyekuwa amekosa karo ya kujiunga na chuo kikuu cha Nairobi kupata mafunzo ya sheria.

Caroline Wanjugu Mwangi 17, alifanya mtihani wa KCSE 2020 katika shule ya upili ya wasichana ya Mahiga na kuzoa alama ya A- (pointi 78) ila familia yake haikuwa na uwezo wa kifedha wa kumpeleka katika chuo kikuu kusomea sheria.

Mwaura amesema kwamba mama ya mwanafunzi huyo alimpigia simu akiomba usaidizi na kupitia muungano wa Albino nchini ambao anaangoza, mwanasiasa huyo akaweza kulipia mwanafunzi huyo karo ambayo ilihitajika.

Baada ya kumaliza kulipa karo mwandani huyo wa naibu rais aliandamana na mwanafunzi yule hadi chuo kikuu cha Nairobi kilicho Parklands.

"Nilichukua muda kuhakikisha kwamba amejiunga na chuo cha sheria cha UON Parklands" Mwaura alisema.

Wanjugu ni kitinda mimba katika familia yao ambapo ndugu zake wawili pia ni zeruzeru.

Mwaura amesema kwamba ndoto ya Wanjugu ni kuwa jaji ili aweze kuhakikisha kuwa wanyonge wamepata haki yao kwani anaelewa jinsi mtu aliyebaguliwa huhisi.

"Tunashukuru Mungu kwa haya na tutaendelea kukubali atutumie kufanya mengi ili tusaidie watu kupata nafasi sawa tunapoendelea kutimiza majukumu yetu" Mwaura alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook.