Majonzi! Mwanaume apoteza mkewe na watoto watatu kwenye mkasa wa moto ulioteketeza nyumba yote Kwale

Muhtasari

•Inaripotiwa kwamba mume wa Bi Samia alikuwa ameenda kutazama mpira wakati  mkasa huo ulitokea.

Moto mkubwa
Moto mkubwa
Image: WIKIPEDIA

Hali ya huzuni imetanda katika  eneo la Taru kaunti ya Kwale baada ya mwanamke mmoja na watoto wake watatu kufariki kufuatia mkasa wa moto ambao uliteketeza nyumba yao usiku wa Ijumaa.

Ripoti ya polisi ilithibitisha kwamba Bi Samia Kikoi ,32, na wanawe watatu; Husnein Hussein,10, Mulhat Hussein,6, na Ilham Hussein,1, waliteketea hadi kifo kufuatia mkasa huo.

Baadhi ya majirani wanaamini kuwa moto huo ulisababishwa na mchumaa ila polisi ambao walifika katika eneo la tukio hawakuweza kuthibitisha chanzo cha moto uliosababisha maafa yale.

Inaripotiwa kwamba mume wa Bi Samia alikuwa ameenda kutazama mpira wakati  mkasa huo ulitokea.

Juhudi za wakazi za kujaribu kuzima moto ule ziliangulia patupu kwani ulikuwa umeenea sana. 

Majirani walijaribu kutumia maji na matawi kuuzima moto ule ambao ulizimika baada ya kuteketeza karibu kila kitu.

Miili ya wanne hao ilipelekwa katika mochari ya Kinango huku uchunguzi zaidi uking'oa nanga.