Upasuaji wa mwili wabaini kilichosababisha kifo cha mama ya DJ Evolve

Familia ilitoa ombi kupewa nafasi ili kuomboleza kifo cha mpendwa wao.

Muhtasari

•Upasuaji wa mwili ambao ulifanywa na mwanapatholijia mkuu wa serikali Johansen Oduor  ulithibitisha kwamba Bi Hongo aliangamia kutokana na tatizo la mwili linalofahamika kama Abdorminal Aortic Aneurysm (AAA) .

Image: HISANI

Mary Hongo, mama ya mcheza santuri Felix Orinda almaarufu kama DJ Evolve  alifariki kutokana na uvimbe moyoni.

Upasuaji wa mwili ambao ulifanywa na mwanapatholijia mkuu wa serikali Johansen Oduor  ulithibitisha kwamba Bi Hongo aliangamia kutokana na tatizo la mwili linalofahamika kama Abdorminal Aortic Aneurysm (AAA) .

Alipokuwa anahutubia wanahabari siku ya Jumamosi, msemaji wa familia Kennedy Ochieng alisema kuwa maradhi ya AAA husababisha uvimbe kwenye mshipa wa damu unasambaza damu kutoka moyoni.

Bi Hongo alizirai  akiwa nyumbani kwao katika mtaa wa Lucky Summer mnamo Septemba 22. Alikimbizwa katika hospitali ya Mama Lucy Kibaki ambako ilitangazwa kuwa alikuwa ashafariki.

Familia ilitoa ombi kupewa nafasi ili kuomboleza kifo cha mpendwa wao.

Kabla ya kifo chake, Bi Hongo ndiye alikuwa anamhudumia mwanawe DJ Evolve ambaye baadhi ya viungo vya mwili wake vililemaa baada ya kupigwa risasi mnamo Januari mwaka uliopita.