Mwanamke anayedaiwa kujaribu kuiba mtoto KNH baada ya kupatikana akiwa amefunga mto tumboni akijifanya mjamzito kuzuiliwa siku zaidi

Muhtasari

•Kulingana na karatasi za mahakama, Shokau alikamatwa mnamo Septemba 23 mida ya saa kumi unusu alasiri akielekea katika wadi ya leba huku akiwa ameweka mto tumboni.

•Hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani Bernard Ochoi aliruhusu polisi kuendelea kumzuia Elizabeth Shokau ili kupatia nafasi uchunguzi zaidi kufanyika. Ochoi alisema kwamba kesi hiyo inahitaji kuchunguzwa zaidi.

court
court

Habari na Carolyne Kubwa 

Mwanamke mmoja aliyepatikana katika hospitali ya Kenyatta akiwa ameweka mto tumboni ili aonekane kama mwenye ujauzito ataendelea kuzuiliwa na polisi kwa siku tatu zaidi.

Hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani Bernard Ochoi aliruhusu polisi kuendelea kumzuia Elizabeth Shokau ili kupatia nafasi uchunguzi zaidi kufanyika. Ochoi alisema kwamba kesi hiyo inahitaji kuchunguzwa zaidi.

Kulingana na karatasi za mahakama, Shokau alikamatwa na koplo Jackline  Makumba mnamo Septemba 23 mida ya saa kumi unusu alasiri akielekea katika wadi ya leba huku akiwa ameweka mto tumboni.

Afisa Makumba aliomba mahakama kupatiana amri Shokau apelekwe katika hospitali ya Mathare ili afanyiwe vipimo vya kiakili kama ilivyopendekezwa na madaktari wa hospitali ya Kenyatta.

Afisa huyo pia alisema kwamba polisi hawakuwa wamekamilisha uchunguzi ili kubaini hali ya ujauzito ya mwanamke huyo ili kujua mashtaka sahihi ya kumshtaki nayo.

Polisi walisema kwamba mshukiwa ameolewa na ako na watoto wawili tayari.

Kulingana na mashtaka yaliyofikishwa mahakamani, inaaminika  kwamba mwanamke huyo alikuwa na nia ya kuiba mtoto.

Kesi hiyo itatajwa tena siku ya Ijumaa.