Mwili wapatikana ukiwa umetupwa ndani ya jengo lisilokamilika Kisumu, wakazi walidhani ni mzigo

Muhtasari

•Watoto ambao walikuwa wamepeleka mifugo malishoni mida ya jioni siku ya Jumapili walipata mwili huo ukiwa umefungwa na kitamba.

crime scene
crime scene

Hali ya hofu ilitanda katika kijiji cha Got Kowino, eneo la Rachuonyo kaunti ya Kisumu baada ya mwili wa kijana kupatikana ukiwa umetupwa ndani ya jengo ambalo halijakamilika.

Watoto ambao walikuwa wamepeleka mifugo malishoni mida ya jioni siku ya Jumapili walipata mwili huo ukiwa umefungwa na kitamba.

Mzee mmoja wa kijiji, Joseph Owino alisema kwamba waligundua mwili ule baada ya kupokea taarifa kutoka kwa watoto ambao walidhani ulikuwa mzigo ambao umetupwa.

Owino alisema kwamba hawakumfahamu marehemu kwani hakuna yeyote aliyekuwa ameripotiwa kupotea katika eneo hilo.

Wanakijiji wametoa ombi kwa wamiliki wa majengo ambayo hayajakamilika kuweka ulinzi ama kuyabomoa kufuatia tukio lile.

Alipokuwa anathibitisha tukio hilo, chifu wa eneo la Kokwanyo Peter Odero alisema kwamba mwili huo ulikuwa umepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Rachuonyo Kusini huku akitoa agizo kwa yeyote ambaye ana taarifa kuhusu tukio hilo kupiga ripoti kwa polisi.