Mshtuko Kirinyaga baada ya mwili wa kitoto kupatikana ukiwa umetupwa kwenye jalala

Muhtasari

•Inaaminika kitendo kile cha unyama kilitekelezwa usiku wa Jumanne kwani kulingana na mkazi mmoja wa eneo hilo, Philip Mwendwa, mwili ule haukuwa pale mwendo wa  jioni alipokuwa anapita.

•Inadaiwa kwamba hilo ni tukio la pili kufanyika pale ndani ya kipindi cha miezi mitatu kwani hapo awali kuna mwili wa mtoto msichana ambao ulipatikana ukiwa umetupwa pale pale.

Polisi akiokota mwili wa kitoto Kerugoya
Polisi akiokota mwili wa kitoto Kerugoya
Image: WANGECHI WANGONDU

Habari na Wangechi Wang'ondu

Polisi katika kaunti ya Kirinyaga wanawinda mtu ambaye alitupa mwili wa kitoto cha takriban miezi saba karibu na kontena ya taka iliyo kwenye viunga vya mji wa Kirinyaga.

Wapita njia ambao walikuwa wanaelekea kazini alfajiri ya Jumatano walipatwa na mshtuko mkubwa kuona mwili wa kitoto cha kiume ukiwa umetupwa pale na kuarifu maafisa wa usalama.

Inaaminika kitendo kile cha unyama kilitekelezwa usiku wa Jumanne kwani kulingana na mkazi mmoja wa eneo hilo, Philip Mwendwa, mwili ule haukuwa pale mwendo wa  jioni alipokuwa anapita.

Mwendwa alisema kwamba alikuwa anaelekea kazini mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi ya Jumatano alipogundua mwili uliokuwa umelala karibu na kontena ya taka na akataka kujua zaidi ndiposa akasonga karibu na kugundua ulikuwa mwili wa mvulana.

Inadaiwa kwamba hilo ni tukio la pili kufanyika pale ndani ya kipindi cha miezi mitatu kwani hapo awali kuna mwili wa mtoto msichana ambao ulipatikana ukiwa umetupwa pale pale.

Chifu wa eneo hilo Justus Mwai alisema kwamba polisi wameanza operesheni ya kuwinda aliyetekeleza kitendo hicho.

Mwili huo ulichukuliwa na polisi kutoka kituo cha Kerugoya na kupelekwa katika mochari ya Kerugoya huku uchunguzi zaidi ukipangiwa kufanywa.