Jamaa azuiliwa kwa kufyatua risasi hewani kutishia kijana aliyefumania akijiburudisha na mkewe garini Kilifi

Muhtasari

•Jamaa huyo mwenye umri wa miaka 47  anaripotiwa kufuata mkewe kutoka nyumbani kwao mjini Mtwapa hadi mkahawa wa Tamaduni Afrika Gardens ambako alifumania mkewe akijiburudisha na mpenzi wake wa miaka 29 ndani ya gari.

crime scene
crime scene

Polisi katika kaunti ya Kilifi wanazuilia jamaa mmoja anayedaiwa kupiga risasi hewani ili kutishia kijana ambaye amekuwa na uhusiano wa kimapenzi na bibiye.

Mmiliki huyo wa bunduki kihalali alikamatwa siku ya Jumamosi baada ya kujisalimisha kwa polisi mwenyewe muda mfupi tu baada ya kutumia bastola yake kutishia kijana anayeaminika kuwa mpango wa kando wa mkewe.

Jamaa huyo mwenye umri wa miaka 47  anaripotiwa kufuata mkewe kutoka nyumbani kwao mjini Mtwapa hadi mkahawa wa Tamaduni Afrika Gardens ambako alifumania mkewe akijiburudisha na mpenzi wake wa miaka 29 ndani ya gari.

Kulingana na ripoti ya polisi, mshukiwa aliposhuhudia yale  alitoa bastola yake aina ya Ceska na kupiga risasi moja hewani ili kutishia kijana yule.

Kufuatia  hayo kijana yule ambaye alikuwa ameingiwa na kijibaridi mwilini aliruka nje ya  gari na kutimua mbio ili kuokoa maisha yake ambayo yalikuwa hatarini.

Baada ya hayo mshukiwa alijisalimisha katika kituo cha polisi ambako bastola yake ilichukuliwa na atashtakiwa kwa kosa la kuhatarisha maisha ya umma.